Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu leo Desemba 11, 2023 amefungua mafunzo ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara yanayofadhiliwa na Mradi wa Afya Thabiti unaotekelezwa na Shirika la AMREF Afrika na kuwataka Waandishi wa Habari kutoa elimu za mapambano dhidi ya UKIMWI.
Akizungumza wakati wa uhufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mwembeni Complex, Dkt Masatu ameeleza kuwa Waandishi wa Habari wanaomchango mkubwa sana katika kuielimisha jamii katika mapambano hayo.
“Jamii ikujua umuhimu wa kupima afya na ikapima na kupokea majibu na ushauri wa wataalamu inaweza kusaidia katika kupunguza maambukizi ya UKIMWI” amesema Dkt. Masatu
Dkt. Masatu ameeleza kuwa ili kufanikiwa kupunguza kasi ya maambukizi katika Mkoa wa Mara, ushirikiano baina ya Serikali, watoa huduma za afya na Waandishi wa Habari unahitajika sana ili kuweze kufikia malengo ya kupunguza maambukizi.
Aidha, Dkt. Masatu amewashukuru sana Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano wanaoutoa katika kutangaza shughuli, Kampeni na miradi mbalimbali ya Sekta ya Afya.
“Dunia inalenga kuwa ifikapo mwaka 2030 kusiwepo maambukizi ya UKIMWI na hili litafanikiwa kama Waandishi wa Habari na vyombo vya Habari vitashiriki katika kuuelimisha umma kuhusu namna ya kujiepusha na maambukizi ya UKIMWI” amesema Dkt. Masatu.
Kwa upande wake Mratibu wa Upimaji UKIMWI na Tohara Kinga Mkoa wa Mara Bwana Felix Mtaki ameeleza kuwa kiwango cha maambukizi katika Mkoa wa Mara kimepanda kutoka asilimia 3.6 miaka mitano iliyopita hadi asilimia 5 mwaka jana.
Bwana Mtaki ameeleza kuwa maambukizi hayo yameongezeka kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
“ Kiwango cha maambukizi kwa Mkoa wa Mara ni kikubwa kuliko kiwango cha kitaifa cha asilimia 4.5” amesema Bwana Mtaki na kuzitaja sababu ya ongezeko hilo kuwa ni pamoja na uwepo wa shughuli za uchimbaji wa madini, uvuvi na mila na tamaduni za wananchi wa Mkoa wa Mara.
Bwana Mtaki ameeleza kuwa baadhi ya makabila hayafanyi tohara kwa wanaume wakati kiutaalamu tohara inasaidia kuepuka maambukizi ya UKIMWI kwa asilimia 60 na hivyo jamii hizi zipo kwenye hatari ya maambukizi zaidi ya UKIMWI.
Aidha, ameitaja sababu nyingine ni kuwepo kwa mtandao wa ngono ambapo watu wengi wanakuwa na wapenzi zaidi ya mmoja na hivyo kueneza maambukizi ya virusi kwa haraka zaidi.
Wakati huo huo, Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Mara Dkt. Omari Gamuya ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha maambukizi mapya yanapungua katika jamii ikiwemo na kampeni za kutoa elimu katika ngazi ya jamii.
Aidha, Mkoa kwa kushirikiana na wadau umeanza kutoa huduma za dawa tiba kwa kutumia alama za vidole ambayo imesaidia kutoa dawa sahihi
Mafunzo ya Waandishi wa Habari ya siku tatu kuanzia tarehe 11 Desemba, 2023 yamehudhuriwa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Shirika la AMREF Afrika na Waandishi wa Habari kutoka baadhi ya vyombo vya Habari vya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa