Mkoa wa Mara leo umeunda timu maalum kwa ajili ya kuchunguza wafanyabiashara waliopewa kibali cha kusambaza sukari ya ruzuku ndani ya Mkoa wa Mara kutoka kwa wafanyabishara waliopewa kibali cha kuingiza sukari nchini.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Mara, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda amewaonya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao walipewa kibali cha kusambaza sukari na kufanikiwa kupata sukari hiyo lakini kuna wasiwasi wa kuiuza bei kubwa ikilinganishwa na bei elekezi ya Serikali au kuficha baadhi ya sukari iliyoidhinishwa kwa ajili ya Mkoa wa Mara.
“Ninawataka wafanyabiashara wote waliopewa vibali vya kusambaza sukari ya ruzuku ndani ya Mkoa wa Mara kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na utaratibu waliokubaliana na Serikali, la sivyo Mkoa utachukua hatua kali dhidi ya wote watakaofanya kinyume na makubaliano” amesema Mhe. Mtanda.
Amewataka wafanyabiashara waliopata vibali hivyo waiuze ndani ya Mkoa wa Mara na kwa bei elekezi iliyowekwa na Serikali na kuwataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kuendelea kupokea maombi ya vibali vya wafanyabiashara zaidi wanaohitaji kuingiza sukari katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda amewataka wafanyabiashara kuacha mara moja tabia ya kupandisha bei za vyakula wakati huu ambapo waumini wa dini za Kikristu na Kiislamu wapo katika mfungo kwa mujibu wa imani zao na kuwataka maafisa biashara kufuatilia mienendo ya bei na kutoa taarifa kwa viongozi mapema ili waweze kuchukua hatua.
Wakati huo huo, Mkoa wa Mara umeunda kikosi kazi cha kupitia mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa wa Mara ili kuuboresha mwongozo uliopo kwa sasa kabla ya kuanza maandalizi ya kampeni ya kuhamasisha uwekezaji kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Akizungumzia suala la sukari, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara na Viwanda Bwana Gambaless Timotheo ameeleza kuwa hadi leo Mkoa umepokea tani 457 za sukari kupitia kwa wakala wa usambazaji mbalimbali ambao wamepeleka sukari katika Wilaya za Bunda na Musoma.
Bwana Timotheo amesema kwa wastani sukari katika Mkoa wa Mara inauzwa shilingi 3,600 hadi 4,500 kwa kilo moja tofauti na maelekezo ya Serikali ya kuuza kilo moja kwa shilingi 2,800 hadi 3,000.
Amezitaja Halmashauri zilizoathirika zaidi na tatizo la upungufu na bei ya sukari kuwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ambazo hazina tatizo la sukari ni Halmashauri ya Mji wa Bunda, Manispaa ya Musoma.
Aidha, Bwana Timotheo amesema baadhi ya wasambazaji ambao wamepokea sukari ya ruzuku kutoka Serikalini hawajaisambaza sukari hiyo Mkoa wa Mara na maghala yao hayajawahi kuuza sukari tokea wao wapokee sukari ya ruzuku.
“Pia kuna udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara kwa kuuza sukari katika bei ya juu tofauti na inavyoandikwa kwenye risiti ya malipo na hivyo kuwafanya wafanyabiashara wadogo kununua sukari kwa bei ya juu” amesema Bwana Timotheo.
Kikao hicho pia kimepokea taarifa mbalimbali ikiwemo hali ya viwanda na biashara katika Mkoa wa Mara, noti bandia na namna kutunza fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), taarifa ya Shirika la Bima la Taifa (NIC), taarifa kuhusu Stakabadhi Ghalani pamoja na kupokea taarifa ya Mamaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, wajumbe wa Baraza hilo, wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, wenyeviti, Wakurugenzi, maafisa biashara, kilimo kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na baadhi ya watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa