Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 26 Juni 2021 ametoa tahadhali ya ugonjwa wa UVIKO 19 (Covid 19 au corona) kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara leo tarehe 26 Juni 2021 katika ukumbi wa uwekezaji, Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima wakati huu ambapo wimbi la tatu la ugonjwa huu likiwa limeingia Tanzania.
“Ninawahimiza wananchi wote wazingatie na kufuata njia kuu za kuzuia maambukizi zilizobainishwa na wataalamu wa Afya na kutokuwa na taharuki” amesema Mheshimiwa Hapi.
Mhehsimiwa Hapi ameeleza kuwa mbalimbali yenye mikusanyiko mfano, mialo, machimbo ya madini mbalimbali, masoko na minada kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kama inavyoelekezwa na watalaam wa afya.
Aidha amewataka wananchi kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara, kutumia vipukushi (sanitizers) mara kwa mara wanapohisi kugusa maeneo/vitu ambavyo havipo salama na kuwapeleka mapema ndugu/jamaa wanaoonesha dalili zinazohisiwa kuwa za UVIKO 19 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate tiba.
Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuvaa barakoa kwa usahihi hasa katika maeneo yenye mikusanyiko, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kupunguza idadi na safari ya ndugu wanaofika kusalimia wagonjwa wodini.
Mkuu wa Mkoa pia amewataka waasimamizi na watumishi wa Sekta ya Afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kutumia kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo matumizi ya vyombo vya habari hususan redio za jamii, mitandao ya kijamii pamoja na vipeperushi vinavyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Aidha amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa huduma kikamilifu bila kuchoka huku wakichukua taadhari zote za kujilinda na wadau wote wa Afya na maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali kutoa msaada wa hali na mali pindi utakapohitajika katika mapambano haya.
Mheshimiwa Hapi amevitaka vyombo vya habari na waadishi wa habari kushirikiana na serikali ili kuwatuliza wananchi kwa kuwapa habari sahihi na kutojuwaletea taharuki.
“Mimi naamini kuwa UVIKO 19 unaepukika kama wadau wote tukishirikiana na kila mmoja kuchukua hatua stahiki za kujikinga zaidi kuondoa hofu na taaruki” amesema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa njia za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vipukushi mikono (sanitizers), kuvaa barakoa hasa katika maeneo yenye misongamano ya watu, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Amezitaja njia nyingine kuwa ni kufanya mazoezi ya viuongo mara kwa mara, ulaji wa mlo ulio kamili na kuzingatia ushauri unaoendelea kutolewa na wataalamu wa afya.
Mkuu wa Mkoa wa Mara ametoa tahadhari hiyo kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan tarehe 25/6/2021 kuwaelekeza viongozi wa dini kuwahimiza na kuhakikisha waumini katika madhahebu yao mara zote wanazingatia kufuata kanuni za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa mapya ya UVIKO 19.
Aidha Marais wa nchi za Kenya na Uganda ambazo Mkoa wa Mara unapakana nazo wameeleza uwepo wa ongezeko la wagonjwa walioambukizwa UVIKO 19 na kuweka mikakati mbalimbali inayolenga kuzuia maambukizi.
Mkoa wa Mara kwa kutambua mwingiliano uliopo baina ya wananchi wan chi hizi tatu umeanza kuchukua tahadhari ya kuzuia maambukizi kwa wananchi wake kama vile kupima homa kwa wasafiri wote wanaovuka mipaka kuingia au kutoka nje ya Mkoa wa Mara; wahisiwa wenye dalili za ugonjwa kupimwa kwa kipimo cha haraka cha UVIKO 19 (rapid test) na kuwekwa kwenye uangalizi.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuhimiza wananchi kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni; kila ofisi iliyoko mpakani kuwa na vipukushi vya kutakasa mikono kwa watumishi na wageni wanaohudumiwa katika ofisi zao.
Mkuu wa Mkoa aliambatana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wawakilishi wa viongozi wa dini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa