Mkoa wa Mara leo tarehe 17 Machi 2020 umetoa mafunzo kwa watumishi wa afya na sekta zinazohudumia wageni ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo yanayotokana na virusi vya Corona (COVID 19) yaliyofanyika katika Chuo cha Matabibu Musoma kilichopo katika Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Florian Tinuga amesema lengo la mafunzo hayo ni kujengeana uwezo wa namna bora ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko husuni yanayotokana na vizuri vya Corona.
“Tunataka mafunzo haya yawe ndio msingi wa kukabiliana na dharura zote za afya katika Mkoa wa Mara na matokeo ya mafunzo ni kupata ujuzi na kuandaa timu za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko”alisema Dkt. Tinuga.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Method B. Mkoba amewataka watumishi wote wanaopewa mafunzo kuzingatia mafunzo hayo ili wakayatekeleze kwa vitendo.
“Ninyi ndio askari wetu tunaowategemea katika vita hii, mnatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa watumishi wenzenu na wananchi kwa ujumla” alisema Bwana Mkoba.
Aidha amewatoa hofu wananchi wote kuwa Mkoa wa Mara kwa sasa ni salama na kuwasistiza wananchi kufuatilia maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na serikali katika kukabiliana na mlipuko wa Corona hapa nchini.
Bwana Mkoba pia ameipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya mpaka sasa tangu mlipuko huu ulipotokea.
“Kazi wanayoifanya ni kubwa sana, hususan ya kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu nini kinachoendelea na tahadhari za kuchukua”.
Wakati huo huo Mtaalamu wa Magonjwa ya Mlipuko Dkt. William Nangi ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana hasa kwa mikoa iliyopembezoni kama Mkoa wa Mara ambayo ni rahisi kuambukizwa na watu wanaotokea nje na ndani ya nchi.
“Sisi tunawaandaa ili wawe na utayari wa kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa wa milipuko ikiwemo magonjwa yanayotokana na virusi vya Corona” alisema Dk. Nangi.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto na kuhudhuriwa na viongozi wa afya wa kila wilaya na Halmashauri, wataalamu wa afya kutoka Uwanja wa Ndege Musoma, mpaka wa Tanzania na Kenya wa Sirari, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kupokea wagonjwa wa milipuko katika Mkoa wa Mara pamoja na wadau wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa