Mkoa wa Mara leo tarehe 4 Mei 2020 umetoa mafunzo ya namna ya kujikinga maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID 19) kwa wafanyakazi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa wafanyakazi wa ofisi hii ili waweze kutimiza wajibu wao wakiwa salama.
“Ninashukuru Katibu Tawala umeamua tuwe na haya mafunzo hapa, maana ugonjwa ukiingia hapa ofisini unaweza kuenea ndani ya muda mfupi sana na watu wengi kama hawatachukua tahadhari wataambukizwa” alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa kwa sasa tunapambana na kirusi ambacho hakijulikani vizuri hata kwa wataalamu wa afya na bado hamna dawa wala tiba ya ugonjwa unaosababishwa na kirusi hicho.
“Muhimu kwetu kwa sasa ni kupokea ushauri na maelekezo yote ya wataalamu wa afya lakini pia kuangalia njia za asili ambazo zimekuwa zikitumika katika kupambana na magonjwa mbalimbali katika jamii zetu” alisema Malima.
Ameeleza kuwa imani za watu pia kwa wakati huu ni muhimu sana, lakini imani isishindane na utaalamu wa kisayansi bali imani iendane na ushauri wa kitaalamu na maagizo ya serikali.
Aidha Mheshimiwa Malima amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha wataalamu wa afya wanatoa elimu kwa watu wanaotengeneza barakoa ili waweze kutengeneza zinazokidhi vigezo vya kuwakinga watu na maambukizi.
Amewataka wafanyakazi na hususani ambao ni wataalamu wa afya kusaidia katika kuwapunguzia hofu walionayo wananchi wengi kwa sababu ya kutokuelewa na uvumi unaoenezwa kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wafanyakazi ili waweze kujikinga na kuwakinga wateja wao wanaowapa huduma.
“Ninachowaomba ni kuyapa umuhimu mkubwa mafunzo haya muda wote tutakapoendelea kuwa na Corona ili tuweze kujikinga na maambukizi haya na ninawataka wafanyakazi wote kuchukulia suala la kujikinga na maambukizi ya Corona kwa uzito mkubwa” alisema Bibi Mthapula.
Ameeleza kuwa leo tumepata elimu ya namna bora ya kuishi na Corona katika mazingira yetu na hususani ofisini ambako ndio tunakaa masaa mengi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Florian Tinuga ameshukuru kwa Katibu Tawala kuona uhumihimu wa kutoa mafunzo hayo kwa wafanyakazi ili waweze kujikinga na corona.
“Mafunzo haya yatatusaidia sisi wafanyakazi kwani yatatuelekeza tunawezeje kuishi na Corona huku tukifanya kazi vizuri” alisema Dkt. Tinuga.
Katika mafunzo hayo wafanyakazi pia wamepitishwa katika miongozo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto na mwongozo wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) juu ya namna ya kuzuia maambukizi ya Corona sehemu za kazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa