Mkoa wa Mara umetoa eneo la ekari 124 katika kijiji cha Nyabange, Wilaya ya Butiama katika fukwe za Ziwa Victoria kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Wanamaji.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua eneo hilo, Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Jenerali Venance Mabeyo ameushukuru Mkoa wa Mara na mmiliki wa awali wa eneo hilo kwa kukubali kutoa eneo hilo kwa ajili ya ulinzi wa nchi.
“Eneo hili ni zuri na kubwa na linakidhi mahitaji ya jeshi kwa sasa, tunashukuru sana” alisema Jenerali Mabeyo.
Akizungumza wakati wa kuonyesha mipaka ya eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Kighoma Malima amesema amefurahi uamuzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuamua kupanua shughuli zake katika Ziwa Victoria na kuweka kikosi kikubwa katika Mkoa wa Mara.
Mhehsimiwa Malima alisema kuwa awali Mara ilikuwa na kikosi kiteule cha wanamaji ambacho kutokana na ufinyu wa eneo na udogo wake hakikuweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Ameeleza pia kutokana na juhudi za pamoja wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama Mkoa wa Mara, Mkoa umefanikiwa kudhibiti uvuvi haramu, magendo ya samaki na kuongeza mapato yatokanayo na Ziwa Victoria. “Kwa sasa hata upatikanaji wa samaki katika Ziwa Victoria hususan kwa Mkoa wa Mara umeboreshwa sana” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima, Mkoa wa Mara ndio wenye eneo kubwa la Ziwa Victoria na raslimali nyingi za ziwa kwa sasa baada ya mgawanyo wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Wilaya ya Rorya ndio wilaya pekee hapa nchini ambayo eneo lake kubwa lipo mwambao mwa ziwa.
“Kujengwa kwa kikosi cha wanamaji hapa Nyabange kutaleta manufaa makubwa ya kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla” Alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa upande wake mmiliki wa awali wa eneo hilo Mzee Samweli Wambura Kishamuri alisema awali yeye alikuwa na eneo la ekari 240 na kati ya hilo ekari 124 ametoa kwa serikali na ekari 116 amebaki nazo mpaka sasa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa