Mkoa wa Mara leo tarehe 18 Desemba 2020 umetangaza matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2021.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina A. Mthapula amesema kati ya wanafunzi 51,822 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu, wanafunzi 40,426 wamefaulu ambayo ni sawa na asilimia 77.98.
“Kati ya wanafunzi wote waliofaulu mtihani huo, wavulana ni 20,950 na wasichana ni 19,476 wakati kuna wanafunzi 11,396 ambao walifanya mtihani huo lakini hawakufaulu” alisema Bibi Mthapula.
Kwa mujibu wa Bibi Mthapula, kati ya wanafunzi wote waliofaulu, wanafunzi 7,804 wamekosa nafasi za kuchaguliwa awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa ambapo mpaka sasa bado Mkoa unahitaji vyumba 156 ili watoto wote waliofaulu waweze kuanza shule.
“Naziagiza halmashauri kuhakikisha kuwa inakamilisha vyumba hivyo kabla ya tarehe 30 Januari 2030 ili wanafunzi wote waliofaulu waweze kujiunga na kidato cha kwanza” alisema Bibi Mthapula.
Hata hivyo alizipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuwa na vyumba vya madarasa vinavyokidhi mahitaji na ziada na kuzitaka halmashauri nyingine za mkoa huo kuiga mfano huo.
“Niwaombe wadau wenye uwezo kutuchangia kupitia halmashauri zetu ili kuweza kukamilisha kazi hii ya ujenzi wa madarasa ili watoto wetu waanze kusoma mapema iwezekanavyo” alisema Mama Mthapula.
Aidha aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima watafanya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu kuanzia kesho tarehe 19 Desemba 2020 katika halmashauri zote za Mkoa huo.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara Bwana Freedence B. Serapion ameeleza kuwa zoezi la usajili wa wanafunzi limefanyika kupitia mtandao ambapo kwa ngazi ya kitaifa matokeo yametangazwa tarehe 17 Desemba 2020 na waziri mwenye dhamana.
“Wanafunzi hawa walianza darasa la kwanza mwaka 2014 wakiwa 62,596 na waliosajiriwa kufanya mtihani wa mwisho ni 51,882 wakati wengine 1,361 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali” alisema Bwana Serapion.
Aidha Bwana Serapion ameeleza kuwa ufaulu wa wanafunzi kwa ngazi ya Mkoa umepanda kwa asilimia 8.24 huku Wilaya ya Serengeti ikiongoza kwa kufanya vizuri zaidi kuliko wilaya nyingine za Mkoa wa Mara katika matokeo ya mtihani huo.
Aidha katika uchaguzi wa ngazi ya taifa wanafunzi 169 wamepangiwa shule za kitaifa ikiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kikao hicha cha uchaguzi wa wanafunzi kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wabunge, madiwani, Meya wa Manispaa ya Musoma, Wakuu wa Wilaya na watendaji wa halmashauri na Mkoa.
Mitihani ya Darasa la Saba kwa mwaka 2020 ilifanyika tarehe 7 na 8 Oktoba na matokeo ya mtihani huo yalitangazwa rasmi tarehe 23 Novemba 2020 na Baraza la Taifa Mitihani (NECTA)
Katika matokeo ya mwaka huu ufaulu wa wanafunzi umeongezeka na Mkoa umeshika nafasi ya 19 kutoka nafasi ya 26 kwa mwaka 2019.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa