Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene leo tarehe 1 Oktoba, 2024 ameanza ziara yake ya siku nne Mkoa wa Mara na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi kwa uongozi wake katika usimamizi bora wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati anawasalimia watumishi katika ukumbi wa uwekezaji, wakati anawasalimia wananchi wa Suguti, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari Mara, Manispaa ya Musoma, Mhe. Simbachawene amesema kutokana na usimamizi mzuri, Mkoa una miradi mizuri ya maendeleo.
“Nimepata taarifa, nimekagua na kuridhika kuwa miradi katika Wilaya ya Musoma kwa kweli imesimamiwa vizuri ina ubora, matumizi ya fedha yanaonekana na inatumika kama ilivyotarajiwa, hongereni sana” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali na kutokana na usimamizi mzuri kazi kubwa imefanyika na miradi iliyotekelezwa ainaonekana ikiwa na ubora.
“Ninakupongeza sana Mkuu wa Mkoa na wasimamizi wote wa miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika vizuri katika kutekeleza miradi hiyo” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene pia ameahidi kupeleka suala la malipo ya mkandarasi anayekarabati na kupanua Uwanja wa Ndege Musoma na wakandarasi wa barabara, ukamilishaji wa jengo la Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na miradi ya hospitali za Halmashauri ili ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyotarajiwa.
Mhe. Simbachawene ameahidi Serikali itaendelea kushughulikia fidia kwa ajili ya wananchi wa Nyatwali, Uwanja wa Ndege Musoma na Shamba la Utegi ili wananchi hao walipwe na waweze kuondoka katika maeneo hayo kupisha miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu kuliko wakati wowote ule.
Mhe. Mtambi amesema Serikali imeleta zaidi ya shilingi trilioni 1.22 tangu awamu ya sita ilipoingia madarakani ambazo zimetumika kutekeleza miradi zaidi ya 279 ya maendeleo katika Wilaya na halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa kila Wilaya ya Mkoa wa Mara ina mradi mkubwa wa maji iliyopo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji wake na itakapokamilika Mkoa utakuwa na wastani mzuri sana wa upatikanaji wa maji mijini na vijijini.
“Katika awamu hii, Mkuu wa Mkoa anagombana na Wakuu wake wa Wilaya kwa nini hawajatumia fedha za utekelezaji wa mradi zilizoletwa, awali ilikuwa Wakuu wa Wilaya ndio wanamfuata Mkuu wa Mkoa kutaka awasaidie kupata fedha za miradi ya maendeleo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Serikali imeleta fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari na ujenzi huo umeanza na unategemewa kukamilika kwa wakati ili wanafunzi watumie miundombinu hiyo shule zitakapofunguliwa Januari, 2025.
“Tutafuatilia kila mradi na kila sehemu ili miradi yote ikamilike na watendaji watakaokwamisha kwa namna moja au nyingine ukamilishaji wa miradi tutamchukulia hatua” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi pia ametumia muda huo kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa