Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Halmashauri hapa nchini (REDEOA) umeupongeza Mkoa wa Mara kwa kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita (ACSEE) mwaka 2023 ambapo Mkoa wa Mara ulifaulisha kwa asilimia 100.
Pongezi za kufaulisha zimetolewa katika mkutano mkuu wa 10 wa REDEOA uliofanyika katika Jiji la Mbeya kuanzia tarehe 15-16 Aprili, 2024 ambapo Mkoa wa Mara ulikabidhiwa cheti cha pongezi.
Cheti cha pongezi kilichotolewa na REDEOA kimesainiwa na Mwenyekiti wake Michael C. Ligola kimeeleza kuwa REDEOA inatambua jitihada zilizofanywa na Mkoa wa Mara katika kuboresha taaluma.
Katika tihani huo, Mkoa wa Mara ulikuwa na jumla ya watahiniwa 3091 ambapo wavulana walikuwa 2002 na wasichana walikuwa 1089 ambapo matokeo yanaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 1720 walipata daraja la kwanza, 1151 walipata daraja la pili, daraja la tatu 216, mtahiniwa mmoja alipata daraja la nne na watahiniwa 15 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara inaonyesha kuwa kwa matokeo hayo Mkoa uliongeza ufaulu kwa asilimia 0.9 ukilinganisha na mwaka 2022 ambapo ulifaulisha kwa asilimia 99.1 .
Aidha, katika matokeo hayo, Shule za Sekondari Bunda na Natta zimefanikiwa kuingia kwenye kumi bora za makundi yao huku Shule ya Sekondari ya Tarime imeongoza kitaifa kwa kuwa na watahiniwa wengi waliofaulu kwa daraja la kwanza baada ya watahiniwa wake 357 kupata daraja la kwanza.
Shule za Sekondari za Natta (Serengeti), Songe (Manispaa ya Musoma) na Buturi (Rorya) wanafunzi wake wote walipata daraja la kwanza na la pili tu.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa asilimia 55 ya watahiniwa wote walichaguliwa kuingia kidato cha tano wakiwa na ufaulu wa daraja la tatu.
Katika matokeo hayo, Halmashauri ya Mji wa Bunda iliongoza kimkoa ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Mji wa Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Halmashauri ambazo hazikufanya vizuri katika matokeo hayo ni Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa