Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewapokea walimu zaidi ya 50 kutoka Chama cha Walimu Zanzibar walio katika ziara ya mafunzo na utalii katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza na walimu hao, Mheshimiwa Mzee amewapongeza walimu hao kwa kufanya utalii wa ndani na kuchagua kuutembelea Mkoa wa Mara wenye vivutio vingi vya utalii na kihistoria ya Taifa letu.
“Mara ni sehemu ambayo ina vivutio vingi vya asili ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuongeza kuwa Mara ndio chimbuko la Tanzania” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara amefurahi sana kuona walimu hao wamekuja kufanya utalii na kujifunza katika Mkoa wa Mara na kuwataka warudi Mara watakapojisikia uchovu na msongo wa mawazo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Mara ambaye ni mwenyeji wa walimu hao Bibi Suzan Shesha amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuweza kuonana na walimu hao pamoja na ratiba za shughuli zake kuwa nyingi.
“Sisi pamoja na wageni wetu tunashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuweza kukutana na walimu hawa, na tunakuahidi tutawatembeza maeneo yote watakayotaka kwenda na kuwapa ushirikiano wakati wote wakiwa katika Mkoa wa Mara” alisema Bibi Shesha.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) Bwana Musa Abdi Hamis ameeleza kuwa ziara yao pamoja na kujifunza kutoka katika shule mbalimbali za Mkoa wa Mara, watatembelea vivutio vya utalii na nyumbani kwa Baba wa Taifa ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhamasisha utalii kupitia filamu ya Royal Tour.
Bwana Hamis ameeleza kuwa katika ziara hiyo, watatembelea shule mbalimbali za msingi, shule za sekondari zinazofanya vizuri sana na zile ambazo hazifanyi vizuri katika mitihani ya Taifa ili kuweza kujifunza.
Aidha, walimu hao wanatarajia kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, maonyesho ya Mara International Expo yanayoendelea katika viwanja vya Mukendo, Manispaa ya Musoma, mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo eneo la Sirari wilayani Tarime, Shule ya Msingi Mkendo aliyosoma Baba wa Taifa na nyumbani kwa Baba wa Taifa.
Walimu hao pia walitoa zawadi za viungo vya Zanzibar mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa na Chama cha Walimu Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa