Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amempokea Balozi wa Sweeden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Macias Ozaki pamoja na viongozi wengine wanaosimamia mradi wa Global Partnership for Education (GPE) Lanes II waliopo katika Mkoa wa Mara kuendelea na ziara yao ya kukagua utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na mradi huo.
Akizungumza katika mapokezi ya ujumbe huo, Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara umesimamia vizuri miradi yote iliyopokea fedha kutoka katika mradi wa GPE Lanes II na kuuhakikishia ujumbe huo kuwa Mkoa utahakikisha fedha zote zinazoletwa kwa baadaye zitatumika vizuri.
“Miradi yote tuliyoitekeleza kutokana na mradi huu imetekelezwa vizuri na mkiitembelea mtaweza kuona mambo makubwa yaliyofanyika kutokana na fedha tulizopokea, na niwahakikishie tukipewa fedha zaidi tutazitumia vizuri kutekeleza miradi” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema ufadhili wa miradi hii unatokana na sera nzuri za kimataifa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tangu ameingia madarakani amefanya jitihada kubwa kukuza diplomasia ya kimataifa.
Mhe. Mtambi ameishukuru nchi ya Sweden kwa ufadhili unaotoa katika miradi mbalimbali na hususan Sekta ya Elimu katika Mkoa wa Mara na kuiomba nchi hiyo kuendelea kuusaidia Mkoa katika sekta za Elimu, Afya na uwezeshaji wa vijana katika sekta za madini na uvuvi msaada ambao amesema utasaidia kukuza uchumi wa endelevu wa wananchi wa Mara.
Kanali Mtambi ameiomba Sweden kuusaidia Mkoa wa Mara katika jitihada mbalimbali zinazochukuliwa kupambana na tatizo la ukeketaji katika jamii ambalo linaharibu maisha na matumaini ya watoto wa kike wa Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.
Mhe. Mtambi amewaomba wafadhili wa mradi wa GPE Lanes II ambao ni nchi 90 duniani pamoja na ufadhili wanaotoa kuja kuwekeza katika Mkoa wa Mara na hususan katika uchimbaji wa madini, utalii, kilimo, huduma na maeneo mengine watakayoona yanafaa kwa uwekezaji.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mhe. Ozaki amesema amefurahi sana kushiriki katika kuitembelea miradi inayofadhiliwa na nchi ya Sweeden na Global Partnership for Education (GPE) ambayo ni muunganiko wa nchi 90 duniani zinazochangia miradi mbalimbali ya elimu yenye lengo la kuboresha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13.
Mhe. Ozaki amesema ziara hii ya siku nne iliyofanyika katika Mikoa ya Arusha na Mara ni sehemu ya ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa washirika wa GPE Lanes II kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania na ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo.
Mhe. Ozaki ameitaka Serikali ya Tanzania kutekeleza adhma yake ya mageuzi katika elimu na hususan utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa ili kuhakikisha kuwa watoto wanaofundishwa katika mtaala huu wanakuwa wanajamii wabunifu, wataalamu na viongozi ambao wanaweza kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.
“Lengo hili linaweza kutimizwa kama kutakuwa na mgawanyo wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuhakikisha walimu wenye sifa wameajiriwa katika shule zote zenye mahitaji ya walimu” amesema Balozi Ozaki.
Mhe. Balozi ameitaka Serikali ya Tanzania kutenga angalau asilimia 20 ya bajeti yake kwa ajili ya elimu na kuhakikisha kuwa fedha zinazotengwa zinatumika kwenye masuala muhimu yatakayowezesha mageuzi katika Sekta ya Elimu.
Mhe. Balozi pia ametembelea miradi katika Manispaa ya Musoma na katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma ambayo ilipokea fedha za kujenga madarasa mawili na matundu vya vyoo 6 na shule hiyo ikaongeza ofisi moja ya walimu kutokana na fedha za mradi huo.
Aidha, ametembelea Shule ya Msingi Mwembeni B ambapo katika shule hiyo, mradi umefadhili Kituo cha Walimu na vifaa vya kufundishia watoto wenye uhitaji maalum na akiwa hapo pia amepata fursa ya kukagua bustani ya mboga mboga inayohudumiwa na watoto wenye mahitaji maalum na kupokea maelezo ya namna watoto hao wanavyojifunza kuhudumia bustani hiyo.
Wageni wengine walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Olukemi Williams, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Charles Wilson Mahera, wasimamizi wa mradi wa GPE Lanes II kutoka Ubalozi wa Sweeden na Uingereza, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Ziara hiyo inategemewa kuhitimishwa kesho ambapo msafara huo utatembelea Shule ya Msingi Bisumwa, Wilaya ya Butiama na Shule ya Msingi Ibwagalilo ambayo ni shule mpya iliyojengwa katika Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa