Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amepokea vifaa vya tiba ya figo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya kitengo cha Figo cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla ya kupokea vifaa hivyo, Mheshimiwa Malima ameishukuru sana serikali kwa kuleta vitaa hivyo katika Mkoa wa Mara ambavyo vitaenda sambamba na uzinduzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambayo inatarajia kuzinduliwa rasmi mwezi Agosti, 2020.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara ninaishukuru sana serikali kwa kutupatia mashine hizi ambazo zimekuja kuimarisha Kitengo cha Figo katika hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Mara” ameeleza Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima amemuagiza mhandisi mkazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha anakamilisha sehemu zitakazofungwa mashine hizo kabla ya tarehe 30 Julai 2020 na kupunguza vizingizio katika utekelezaji wa mradi huo.
“Serikali imeleta pesa shilingi bilioni 4.1 za kukamilisha mradi huu, sasa fanyeni kazi usiku na mchana kukamilisha ili wananchi waanze kupatiwa huduma haraka iwezekanavyo” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha amemuagiza Katibu Tawala Msaidizi, Miundombinu Mhandisi Faustine Tarai kuhakikisha huduma za umeme, maji na barabara zinafika katika hospitali hiyo kabla ya tarehe 30 Julai 2020.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima kitengo cha Figo na sehemu ya Mama na Mtoto zinatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo tarehe 15 Agosti, 2020 hivyo huduma hizo ni muhimu kuimarishwa mapema.
Kwa upande wake Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza Dkt. Frederick Buswelo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee ambaye alikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya serikali ameeleza kuwa vifaa vilivyoletwa ni Mashine tisa za kusafisha figo, vitanda tisa pamoja na vifaa vya kufundia mashine hizi.
Dkt. Biswalo ameeleza kuwa vifaa hivi ni sehemu ya mashine 62 zilizotolewa na Serikali ya Falme za Kiarabu aidha shirika moja la Ujerumani liliongeza nyingine ambazo zimegawiwa katika hospitali za rufaa mbalimbali Tanzania bara pamoja na Zanzibar.
Ameitaja baadhi ya hospitali za rufaa zilizopata mashine hizi ni pamoja na Mara, Tanga, Mwanza, Kigoma, Mtwara na kadhalika na kuwa mpango wa serikali kupeleka mashine hizi katika hospitali za rufaa 20 ifikapo Novemba 2020.
“Upatikanaji wa vifaa hivi katika hospitali zetu za rufaa itapunguza sana gharama za kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata huduma hizo na itaokoa vifo vingi sana hususan kwa wanawake wajawazito.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Mkoa wa Mara Dkt. Joakim Enyembe ameeleza kuwa maandalizi ya kupokea vifaa hivi ikiwa ni pamoja na kuwaandaa watumishi watakaosimamia yamefanyika.
“Tayari hospitali imetoa wafanyakazi saba ambao wameshapatiwa mafunzo ya kuvtumia na baada ya kufungwa wataanza kuvitumia” alisema Dkt. Enyembe.
Ameeleza kuwa vifaa hivi vitaokoa maisha ya wananchi walio wengi katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa