Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo ametoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mapokezi ya vifaa tiba kwa ajili ya kutolea huduma za afya na magari 31 ya kubebea wagonjwa na usimamizi wa sekta ya afya katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara ofisini kwake, Mhe. Mtanda amesema Mhe. Rais ameleta magari ya kubebea wagonjwa 20 na magari ya usimamizi wa sekta ya afya 11 na kati ya magari hayo, tayari magari matatu yameshapokelewa katika katika baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Mara.
“Katika mgawanyo wa magari hayo, kila halmashauri itapata magari mawili ya wagonjwa na gari moja ya usimamizi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara pia itapata magari mawili ya wagonjwa na gari moja la usimamizi, na ofisi yangu itapokea gari moja kwa ajili ya usimamizi” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Mheshimiwa Mtanda ameeleza kuwa kwa sasa huduma za afya katika Mkoa wa Mara zimeimarika ambapo Hospitali zote za Halmashauri zimeanza kufanya kazi na huduma zinaendelea kuboreshwa zaidi baada ya mapokezi ya vifaa hivi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Serikali Mkoani Mara imefanikiwa kuwakamata wezi waliokuwa wanajihusisha na wizi wa vifaa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kukamata baadhi ya vifaa vilivyoibiwa kwa nyakati tofauti tofauti.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa vifaa tiba na magari hayo yanakuja kuimarisha zaidi utoaji wa huduma katika sekta ya Afya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa