Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo amepokea nyumba ya walimu, mradi wa maji na ufadhili wa wanafunzi wenye jumla ya thamani ya shilingi 222,500,000 kutoka Shirika la Zawadi Project.
Akizungumza katika hafla ya kupokea msaada huo, Mheshimiwa Mzee amelipongeza shirika hilo kwa msaada huo ambao unaisaidia jamii katika shule mbalimbali za Serikali katika kata saba za Tarafa ya Chamriho, Wilaya ya Bunda.
Miradi iliyopokelewa ni nyumba ya walimu yenye uwezo wa kuchukua familia sita yenye thamani ya shilingi 120,500,000/=, mradi wa kisima, matenki na mtandao wa maji wenye thamani ya shilingi 49,000,000/= na ufadhili wa wanafunzi 256 wa shule za msingi na sekondari wenye thamani ya shilingi 53,000,000/=
Akiwa katika eneo hilo, Mheshimiwa Mzee amezindua mradi wa maji katika Shule ya Msingi Kambarage na nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Sarawe zilizojengwa kwa nguvu ya wananchi na ufadhili wa shirika la Zawadi Project.
Mheshimiwa Mzee amemtaka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage kubuni namna ya kukifanya mradi wa maji waliopewa na Shirika la Zawadi kuwa endelevu na kuweza kuleta manufaa yaliyotarajiwa.
Awali, Mratibu Mkazi wa Shirika la Zawadi Project Bwana Nelson Mafie ameeleza kuwa Shirika hilo linafanya miradi yenye lengo la kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu, kuboresha mazingira ya shule na kutoa mafunzo ya walimu kazini.
Kwa mujibu wa Bwana Mafie, miradi iliyopokelewa leo ni mwendelezo wa miradi mbalimbali ambayo shirika hilo limekuwa likiitekeleza katika kata mbalimbali za Tarafa ya Chamriho, Wilaya ya Bunda.
Bwana Mafie ameeleza kuwa ufadhili wa wanafunzi ni kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao.
Kwa mujibu wa Bwana Mafie ameeleza kuwa kwa sasa shirika linawafadhili jumla ya wanafunzi 256 ambapo kati yao wanafunzi 141 wapo shule za msingi, 115 wapo shule za sekondari 14 wapo Kidato cha Tano na Sita, 12 wapo katika mafunzi ya ufundi, 4 wapo vyuo vya kati na 7 wapo katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini.
Bwana Mafie ameeleza kuwa shirika hilo lenye makao yake makuu katika Mkoa wa Arusha, Katika Mkoa wa Mara Shirika hilo linafanya shughuli zake katika Wilaya ya Bunda Tarafa moja ya Chamriho.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa