Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameliomba Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwekeza zaidi katika Shamba Darasa la Mkoa wa Mara maarufu kama viwanja vya Mama Maria Nyerere vilivyopo katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Butiama.
Mheshimiwa Malima ametoa ombi hilo leo tarehe 16 Desemba 2020 ofisini kwake baada ya kumpokea Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge ofisini kwake akiwa katika ziara ya kutembelea Mkoa wa Mara.
“Kwa Mkoa wa Mara tungefurahi sana kama jeshi letu lingewekeza zaidi katika eneo tulilowatengea katika viwanja vya Mama Maria Nyerere ili wananchi wa Mkoa wa Mara waweze kujifunza na kufaidika na utaalamu wa kilimo uliopo JKT” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima amesema kuwa Mkoa uliamua kuanzisha shamba hilo ili kuweza kuwafikia wakulima wake kiurahisi zaidi katika kuwapa elimu, teknolojia na mifano ya kilimo bora kutoka kwa wataalamu na wakulima waliofanikiwa.
“Bado tunaendelea kushiriki katika maonyesho yanayofanyika katika viwanja vya maonyesho ya kilimo kwa Kanda ya Ziwa Mashariki kule Nyakabindi, Simiyu lakini shamba hili ni fursa kubwa zaidi kwa wakulima wetu maana hapa ni karibu na wanaweza kufika na kujifunza” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha amemshukuru Mkuu huyo kwa kazi kubwa ambayo JKT inaifanya katika kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati na hususan kahawa, pamba na mihogo katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Meja Jenerali Mbugi ameeleza kuwa JKT kwa sasa imewekeza sana katika kilimo cha mazao mbalimbali hapa nchini na kwa sasa imeajiri watu sita ambao ni raia waliobobea katika utaalamu wa kilimo.
“Tumepata mafanikio makubwa sana kutokana na uwekezaji katika kilimo na kuliwezesha jeshi kununua magari 27 na matrekta 10 kutokana na fedha za ndani” alisema Mkuu wa JKT.
Alisema kwa mwaka huu, JKT imewekeza zaidi katika kilimo katika mikoa na mazao mbalimbali ili kuweza kutoa mafunzo ya kilimo kwa wakulima na kuongeza mapato ya ndani ya jeshi hilo.
Ameahidi kuwa JKT itaongeza uwekezaji wake katika eneo walilopewa katika viwanja hivyo ili kutoa mafunzo kwa wakulima na kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mkoa wa Mara umeanzisha maonyesho ya kilimo katika viwanja vya Mama Maria Nyerere kuanzia mwaka huu ili kutoa mafunzo endelevu kwa wakulima kuhusu mazao ya kimkakati ya chakula na biashara ili kuongeza tija kwa wakulima wake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa