Mkoa wa Mara umepata ufaulu wa asilimia 100 katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita kwa mwaka 2023 yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) hivi karibuni.
Akizungumza katika kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kaimu Katibu Tawala sehemu ya Elimu na Ufundi Bwana Makwasa Bulenga ameeleza kuwa kwa mwaka 2023 Mkoa wa Mara umeongeza ufaulu kwa asilimia 0.9 kutoka ufaulu wa asilimia 99.1 wa mwaka 2022.
“Kati ya wanafunzi wote 3091 waliofanya mtihani katika Shule za Sekondari 28, wanafunzi 3090 wamepata daraja la kwanza hadi la tatu na mwanafunzi mmoja tu amepata daraja la nne na hivyo wote wamefaulu” amesema Bwana Bulenga.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa katika Shule ya Sekondari ya Bunda wanafunzi 121 walipata daraja la kwanza ambao ni asilimia 95 ya wanafunzi wote 126 waliofanya mtihani katika shule hiyo na kufanikiwa kupata GPA ya 1.7143 na kushika nafasi ya kwanza katika Mkoa wa Mara.
Aidha, Bwana Bulenga ameeleza kuwa kwa mujibu wa matokeo hayo, Shule za Sekondari ya Bunda na Natta zimefanya vizuri na kufanikiwa kuingia kwenye kumi bora kitaifa katika makundi yao.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa Shule ya Sekondari ya Tarime imeongoza Kitaifa kwa kuwa na wanafunzi wengi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza ambapo jumla ya watahiniwa 357 walipata daraja la kwanza kati ya wanafunzi 498 waliofanya mtihani katika shule hiyo.
“Katika Shule za Sekondari za Natta, Songe na Buturi wanafunzi wake wote waliofanya mtihani huo wamepata daraja la kwanza na la pili tu” amesema Bwana Bulenga.
Akifafanua kuhusu watahiniwa hao, Bwana Bulenga ameeleza kuwa asilimia 55 ya watahiniwa hao walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2021 wakiwa na ufaulu wa daraja la tatu na katika matokeo ya kidato cha sita wamepata daraja la kwanza na la pili.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa ufaulu huo ni matokeo ya mkakati maalum wa Mkoa wa Mara wa kutokomeza daraja la nne na sifuri katika ufaulu wa mitihani ya Taifa.
Bwana Bulenga ameeleza kuwa katika Shule ya Sekondari ya Bunda wanafunzi 121 walipata daraja la kwanza ambao ni asilimia 95 ya wanafunzi wote 126 waliofanya mtihani huo na kufanikiwa kupata GPA ya 1.7143 na kushika nafasi ya kwanza katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara imeipongeza Sehemu ya Elimu na Ufundi, Halmashauri, Walimu na wanafunzi waliofanya mtihani huo kwa jitihada zao zilizowezesha kupata matokeo mazuri katika mtihani huo.
Aidha, Menejimenti imeitaka Sehemu ya Elimu na Ufundi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu katika Mkoa wa Mara kuendeleza ufaulu huo kwenye matokeo ya mitihani ya Taifa ya shule ya msingi, kidato cha pili na cha nne.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa