Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Allu Salum Hapi leo tarehe 22 Juni 2021 amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika Sekondari ya Robanda iliyopo katika Kijiji cha Robanda katika Pori la Akiba la Ikilongo pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani Mara utatembele, Kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi ya maendeleo 50 na kuwasha Mwenge wa Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Mkoa wa Mara ndio mwasisi wa Mwenge wa Uhuru kupitia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa hivyo leo Mwenge wa Uhuru umerudi nyumbani” alisema Mheshimiwa Hapi.
Baada ya mapokezi hay, Mheshimiwa Hapi aliukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Dkt. Vincent Mashinji na kuanza kuukimbiza katika Wilaya ya Serengeti.
Ukiwa katika Wilaya ya Serengeti, Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa maji katika Shule ya Sekondari Robanda; umeweka jiwe la msingi katika mradi wa lambo la mifugo; umezindua ofisi ya Kijiji cha Park Nyigoti; umefungua zahanati ya kijiji cha Koreri; pamoja na kutembelea kitalu cha miche na kuzindua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa katika Shule ya Sekondari ya Kitunguruma.
Aidha Mwenge wa Uhuru umefungua Kituo kidogo cha Polisi cha stendi mpya ya Mugumu; umekagua mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya hospitali (GOTHOMIS) katika Hospitali ya Nyerere (DDH) na umetembelea mradi wa barabara ya lami na kukagua shughuli za vijana zinazofanywa na kikundi cha Bloom Youth Group mjini Mgumu.
Hata hivyo Mwenge wa Uhuru umeukataa mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Robanda kutokana na mapungufu mbalimbalimbali.
Kauli mbiu ya mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu “TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu: Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 17 Mei 2021 katika Mkoa wa Kusini Unguja na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana Kitaifa 2021 itafanyika mkoani Geita tarehe 14 Oktoba 2021.
Katika Mkoa wa Mara Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kuanzia leo hadi tarehe 27 Juni 2021 na tarehe 28 Juni 2021 utakabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa