Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula leo tarehe 29 Aprili 2020 amekabidhi kituo cha Kulelea Watoto cha Musoma Children’s Home kwa Sista Hellena Ntambulwa.
Akizungumza katika makabidhiano rasmi ya kituo hicho, Bibi Mthapula ameeleza kuwa anategemea kituo hicho kitatunzwa vizuri kama kilivyo sasa na kitaboreshwa pale inapohitajika.
“Ni matumaini yetu kuwa kituo hiki kitatunzwa kipendeze kama ilivyo sasa na kuboreshwa endapo maboresho yatahitajika kwa mujibu wa mkataba” alisema Bibi Mthapula.
Aidha amemtahadharisha Sista Hellena kupata usajili wa kituo hicho kabla ya kuanza kutumika tena kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Kwa upande wake Sista Hellena ameshukuru uamuzi wa uongozi wa Mkoa wa Mara wa kuwapatia kituo hicho ili aweze kuendelea kulea watoto yatima.
Sista Hellena ambaye aliambatana na baadhi ya watoto na walezi wa watoto hao ameshukuru ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi wa Mkoa wa Mara tangu alipoonyesha nia ya kuendesha kituo hicho.
Sista Hellena ni mmiliki na msimamizi wa kituo cha Bikira Maria ambacho kinatunza watoto wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na wenye ulemavu wa ngozi, kilichopo Lamadi, wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu.
Kituo cha Musoma Children’s Home ni kituo cha serikali kilianzishwa na Mama Lisbeth Granrundu na mumewake Bwana Danel Granrud ambao wamestaafu na kukirudisha kituo hicho serikalini Januari 2020. Kituo kipo katika eneo la Bweri, Kiwanja Na. 58, Kitalu D chenye ukubwa wa hekta 6.64 pamoja na nyumba sita na mali mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa