Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo ametoa taarifa ya mafanikio ya kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Sisi katika Mkoa wa Mara tumepata mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita na kuiwezesha Serikali kuwaletea wananchi maendeleo katika Nyanja za kiuchumi na kijamii” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa katika kipindi hiki watumishi 8,148 wa Mkoa wa Mara wamepandishwa vyeo huku watumishi 257 wamebadilishiwa kada jambo ambalo limeongeza ari kwa watumishi na kuwafanya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, hadi kufikia Februari, 2022, Halmashauri za Mkoa wa Mara zimetoa mikopo kwa vikundi 187 yenye thamani ya shilingi 1,117,587,995 sawa na asilimia 97 ya fedha iliyopaswa kutolewa kutokana na makusanyo ya ndani.
“Vikundi viivyonufaika na mikopo hii ni vikundi 92 vya wanawake, vikundi 53 vya vijana na vikundi vya watu wenye ulemavu 42” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umetengewa jumla ya shilingi bilioni 22. 469 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu (shilingi bilioni 14.32), afya (shilingi bilioni 6.88) na maji (shilingi bilioni 5.78).
“Katika miradi ya afya, shilingi bilioni 4.803 ni kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na shilingi bilioni 2.08 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara pia umetengewa shilingi billioni 8.362 fedha za ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali za Hamashauri za Wilaya ya Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Tarime (Nyamwaga) na Serengeti; ujenzi wa vituo vya afya 15 na ukamilishaji wa zahanati 26 na nyumba 3 za watumishi.
Aidha katika kipindi hiki Mkoa wa Mara umepokea shilingi bilioni 3.750 zinazotokana na miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 10 kwa ajili ya kujenga majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), maabara, kichomea taka, jengo la kufulia, mionzi, nyumba ya watumishi (3 in 1), na njia za kupita (walkways).
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kimkoa umeongezeka na kufikia asilimia 92.3 hadi Mwezi Machi, 2022 na hii imetokana na Halmashauri kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya manunuzi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Kwa upande wa elimu, Mkoa umepokea shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Sekondari za kata mpya 10 kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na ujenzi wa miradi hii unaendelea.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umepokea jumla ya shilingi bilioni 13 kwa ajili ya Mpango wa ElimuMsingi bila Malipo tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.
Aidha Mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 8.107 fedha za miradi ya maendeleo ya elimu kutoka Serikali Kuu, EP4R, SRWSS, na GPE-Lanes kwa ajili ya miradi mbalimbali ya elimu.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa katika sekta ya Maji, upatikanaji wa huduma za maji safi ni za uhakika na kwa sasa miradi kadhaa inaendelea kutekelezwa ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini na vijijini.
Miradi hiyo ni mradi wa ujenzi wa tanki la Bhalima na miundombinu ya kusafirisha maji (shilingi bilioni 8.5); mradi wa ujenzi wa chujio la Maji katika Mji wa Mugumu (shilingi bilioni 3.121); mradi wa ujenzi wa chujio la maji Bunda Mjini (shilingi bilioni 10.6); mradi wa usambazaji wa maji katika vijiji vya Mbalibali na Kitunguruma katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (shilingi milioni 748.501); mradi wa ukarabati wa miundombinu yam aji katika Mji wa Shirati (Rorya) (shilingi milioni 409); mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari- Butiama (shilingi bilioni 70.863).
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa ili kuboresha huduma za maji vijijini Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara imekamilisha miradi yam aji 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 15 ambayo inahudumia vijiji 193 na kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 59.1 hadi asilimia 65.6.
“Kwa mwaka huu wa fedha RUWASA imetengewa shilingi bilioni 19.757 kwa ajili ya kutekeleza miradi 65 ambapo miradi 29 ni miradi mipya, 12 ni miradi ya upanuzi, 17 ni miradi ya ukarabati wakati o7 ni miradi ya utafutaji wa vyanzo vya maji” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kwa kwa upande wa sekta ya nishani, upatikanaji wa umeme katika maeneo ya mjini ni wa uhakika na kupitia mradi wa REA, jumla ya vijiji 407 vimepata umeme na vijiji 45 vipo katika Mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao utagharimu shilingi bilioni 9.4.
Katika Sekta ya Madini, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2022 Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa imekusanya dhahabu kilo 9,970.68 yenye thamani ya shilingi 1,017,594,887,992.08, madini ya ujenzi yenye tani 16,426.86 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.070; na makenikia ya dhahabu kilo 475,130 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.948.
“Aidha katika kipindi hiki, jumla ya kilomita za mraba 103.871 zimetengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na jumla ya lesseni 213 za uchimbaji mdogo wa madini zimetolewa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Kwa upande wa barabara zinazosimamiwa na Mamlaka ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), jumla ya shilingi bilioni 25.667 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara na vivuko katika serikali za mitaa.
“Hadi kufikia Machi, 2022 jumla ya mikataba 87 ya ujenzi na ukarabati wa barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 21.961 imesainiwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji” alisema Mheshimiwa Hapi.
Kwa upande wa Barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), Mheshimiwa Samia ameongeza bajeti ya barabara kutoka shilingi bilioni 21.82 hadi kufikia shilingi bilioni 22.08.
“Aidha Serikali imetenga fedha za ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma utakaogharimu shilingi bilioni 35.048 na malipo ya fidia kupisha upanuzi wa uwanja kwa wakazi 86 kiasi cha shilingi bilioni 4.337” alisema Mheshimiwa Hapi.
Rais wa awamu ya sita aliapishwa tarehe 19 Machi 2021 kuwa Rais wa Awamu ya Sita mara baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa