Mkoa wa Mara umeanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kufanya vizuri katika matokeo ya wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ili kurejea katika nafasi yake ya zamani.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bwana Benjamin Oganga, wakati akifungua mafunzo ya takwimu kwa walimu wa takwimu wa Shule za Msingi na Sekondari yanayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma.
“Sio jadi yetu Mkoa wa Mara kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani, mimi nimesoma Mkoa Mara elimu ya Msingi na Sekondari na Mkoa wa Mara wakati huo ulikuwa tunafanya vizuri sana, haiwezekani sasa tukawa tunafanya vibaya” alisema Oganga.
Bwana Oganga ambaye pia ni Afisa Eimu wa Mkoa wa Mara ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha walimu waliohudhuria mafunzo hayo kutimiza wajibu wao kwa kufundisha na kuwasimamia wanafunzi katika shule zao.
“Tumepewa dhamana kubwa sana, sisi ndio tunaotengeneza Tanzania, ukisikia viongozi , wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi wote wametengenezwa na walimu, tutimize wajibu wetu” alisema Bwana Oganga.
Bwana Oganga ameeleza kuwa hakuna kazi isiyokuwa na changamoto, hivyo amewataka walimu kutimiza wajibu wao wakati serikali ikizifanyia kazi changamoto zilizopo katika sekta ya elimu ili kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia.
Amewataka walimu kuongeza juhudi katika ufundishaji na ujifunzaji na Mkoa ukibaini kuwa Mwalimu hafundishi utachukua hatua kali ili iwe fundisho kwa walimu wengine.
Kuhusu mafunzo hayo, Bwana Oganga amewakumbusha walimu kuwa kazi ya takwimu wanayoifanya ni kazi ya kisheria na mafunzo hayo yanalengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Bwana Oganga amewasistiza walimu hao kuhusu umakini katika ujazaji wa madodoso mbalimbali yanayoletwa na kuhakikisha usahihi wa takwimu hizo na kuyajaza madodoso na kuyarudisha kwa muda unaotakiwa.
“Tukisema madodoso haya yafike Halmashauri tarehe fulani, basi yajazwe kwa usahihi na yafike kwa tarehe hiyo au kabla ya tarehe husika” alisema Bwana Oganga.
Aidha Bwana Oganga amewataka Maafisa Elimu wa Halmashauri kuwaandikia barua rasmi za uteuzi kwa walimu wote walioshuriki katika mafunzo hayo kwa ajili ya kutekeleza majukumu hayo ikieleza majukumu yao kama walimu wa Takwimu katika shule zao.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Mara Bwana Ayoub Mbilinyi, amemkaribisha Kaimu Katibu Tawala Mkoa kufungua mafunzo hayo.
Bwana Mbilinyi ameeleza kuwa mafunzo hayo ya siku moja yanawahusisha walimu wa Takwimu wa Shule za Msingi na Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma na kesho yataendelea katika halmashauri nyingine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa