Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 22 Oktoba 2021 amezungumzia namna Mkoa wa Mara unavyojipanga katika kuwarahisishia watalii wa ndani na nje ya nchi kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mheshimiwa Hapi ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuzungumzia ushindi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama hifadhi bora ya Afrika kwa mwaka wa tatu mfulilizo.
“Serikali kwa sasa inaendelea kuupanua Uwanja wa Ndege wa Musoma ili ndege za abiria ziweze kutua, aidha mchakato wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mugumu unaendelea ili ndege nyingine ziweze kutua katika uwanja huo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa lengo la kuimarisha viwanja vya ndege nje ya hifadhi ni kwa ajili ya kupunguza ndege zinazotua hifadhini aidha kuruhusu ndege za abiria kuweza kutua karibu kabisa na hifadhi ili kuwavutia watalii wa kipato cha kati na cha chini kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amezungumzia pia barabara za kuingia katika Wilaya ya Serengeti zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na hivi vyote vikikamilika itawarahisishia watalii kuingia na kutoka Serengeti.
“Tunafahamu kuwa sio watalii wote ni matajiri, ndio maana serikali inataka kurahisisha usafiri wa kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kuvutia watalii wengi zaidi hususan wanafunzi, wastaafu na watu wenye uwezo wa kawaida” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kutokana na uwekezaji huo wa serikali, wananchi wa Mkoa wa Mara wanatarajiwa kufaidika aaidi na fursa zitokanazo na utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuliko ilivyo kwa hivi sasa ambapo watalii wengi wanapitia katika mikoa ya Mwanza na Arusha.
Aidha Mheshimiwa Hapi ameipongeza Hoteli ya Four Seasons Safari Lodge ambayo pia imepata ushindi katika tuzo hizo kama hoteli bora.
“Sisi kama Mkoa tunayo agenda kubwa ya kuendelea kuvitangaza vivutio vya utalii lakini pia kuifanya Tanzania na Dunia ijue kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni moja katika urithi mkubwa wa dunia ipo katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshiwa Hapi amempongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutangaza utalii wa Tanzania na pamoja na mkakati wake wa kitaifa wa kuhakikisha tunakuwa na filamu itakayoitangaza Tanzania kimataifa umeanza kuzaa matunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa