Mkoa wa Mara umejipanga kuwapokea wageni mbalimbali watakaokuja kushiriki kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ziara ya Mheshimiwa Rais kuanzia tarehe 4-7 Februari, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ametoa kauli hizo leo tarehe 1 Februari, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Mkoa unatarajia kupokea wageni takriban 5,000 katika kipindi hiki na niwahakikishie watapata huduma za malazi, usafiri, mawasiliano na mahitaji mengine muhimu wakati wote wakiwa Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewahakikishia watanzania kuwa tayari uongozi wa Mkoa wa Mara umefanya mazungumzo na wafanyabiashara mbalimbali wanaotoa huduma na kuwataka watoe huduma kwa weredi, usafi na viwango vinavyokubalika wakati huu.
“Tumeamua katika kipindi hiki chote baa, kumbi za starehe na sehemu za chakula zitanyakazi kwa masaa 24 ili kuwawezesha wageni kupata huduma kiurahisi zaidi wakati wote wanapohitaji” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara kutumia fursa hii kikamilifu ili kuweza kujitangaza na kujiimarisha katika biashara zao na hususan biashara za huduma mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, amewahakikishia wageni wote kuwa Mkoa wa Mara upo salama siku zote na wakati wote wa ziara ya Mshehimiwa Rais itafanyika kwa utulivu na amani.
Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuwasaidia wageni mbalimbali watakaohitaji kujua kuhusiana na maeneo muhimu na sehemu za kupata huduma mbalimbali.
“Mimi ninajua kuwa wananchi wa Mkoa wa Mara ni wakarimu na wanapenda sana wageni hivyo sina mashaka kwamba wageni watapokelewa vizuri katika ziara hiyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewahimiza wananchi wote kuishi kwa amani, upendo na utulivu wakati wote ambapo Mkoa una wageni ili wageni wakalitangaze vyema jina la Mkoa wa Mara huko waendako.
Wageni wanaotarajia kushiriki ziara hii ya Mheshimiwa Rais ni pamoja na Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Viongozi wa Kitaifa waliostaafu, viongozi na makada wa Chama cha Mapinduzi, Wabunge, Viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyabiashara, wanachama wa CCM na wananchi wa kawaida.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa