Mkoa wa Mara umejipanga tayari kwa kupokea mbio za kitaifa za Mwenge wa Uhuru mapokezi yatakayofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Robanda katika Kijiji cha Robanda kilichopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Baada ya mapokezi ya Mwenge utaanza kukimbizwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara hadi tarehe 05 Julai 2022 utakapohitimisha katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na baadaye kukabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara inaonyesha kuwa Mwenge ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti utaweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kijiji cha Robanda; utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Morotonga; utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi Kituo cha Afya Kenyana na kupokea taarifa ya mradi wa kupambana na malaria.
Aidha Mwenge utazindua madarasa katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Mapinduzi na itazindua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa, utafungua kiwanda cha Lumuye Leopard and Hardware; utatembelea kikundi cha vijana magido na kufanya mkesha wa Mwenge katika eneo la Stendi ya Zamani katika Mji wa Mugumu.
Tarehe 28 Juni, 2022 Mwenge utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na makabidhiano yanatarajiwa kufanyika katika eneo la Gibaso na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Itiriyo; kuzindua klabu ya rushwa katika Shule ya Sekondari Nyamwigura; kuweka jiwe la msingi katika daraja la Kebweye na kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Bumera.
Aidha Mwenge wa Uhuru utateketeza madawa ya kulevya katika eneo la Turugeti-Runyerere; kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha mafuta ya alizeti Gwitiriyo; kuweka jiwe la msingi katika Shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Sirari; kutembelea kikundi cha vijana Sirari na kufanya mkesha katika Uwanja wa Tarafa Sirari.
Ratiba hiyo imeonyesha kuwa tarehe 29 Juni, 2022 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na makabidhiano yatafanyika katika Mtaa wa Kogesenda Kata ya Nkende baada yah apo Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Sabasaba; utatembelea klabu ya wapinga rushwa na utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi Gitcheri Sekondari.
Aidha Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ketare; kutembelea kikundi cha vijana katika Barabara ya Nyamwaga; kutembelea mradi wa Halmashauri wa kufyatua tofali na mkesha utakuwa katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Tarime.
Tarehe 30 Juni, 2022 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambapo makabidhiano yatafanyika katika uwanja wa Osogo na baada yah apo kutembelea shughuli za vijana Utegi; kukagua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa katika Shule ya Sekondari ya Nyanduga na kuzindua madarasa ya Shule ya Msingi Tanu.
Aidha Mwenge utazindua mradi wa maji Nyarombo; utaweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Nyamagaro; utakagua shughuli za utengenezaji wa vyakula vya lishe bora katika Hospitali ya Shirati; utakagua mpango wa anuani za makazi katika eneo la Shirati; utateketeza madawa ya kulevya katika Kituo cha Polisi Shirati na Mwenge unatarajia kufanya mkesha katika Mji wa Shirati.
Tarehe 01 Julai, 2022 Mwenge utakimbizwa katika Manispaa ya Musoma na makabidhiano yatafanyika katika kituo cha mabasi Bweri baada ya hapo Mwenge utaweka jiwe la msingi katika daraja la barabara ya Bweri-Kwangwa, utazindua klabu ya wapinga rushwa katika Shule ya Sekondari Musoma; kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Rwamlimi na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa tanki la maji Kwangwa.
Ukiwa Manispaa ya Musoma Mwenge pia utaweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari Kigera; kutembelea shughuli za kikundi cha Nguvu ya Msichana katika eneo la Mwisenge na baadaye kufanya mkesha katika viwanja vya Shule ya Msingi Kigera.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo tarehe 02 Julai, 2022 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na makabidhiano yatafanyika njia panda ya Zahanati ya Mkirira na Mwenge utazindua barabara ya Kwangwa-Mkirira; kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Zahanati ya Mkirira na kutembelea mradi wa ukodishaji wa ukumbi na viti cha Jitahidi Ufaidike katika Shule ya Sekondari ya Mkirira na kugawa bima ya afya ya jamii kwa wazee na watu wenye ulemavu.
Aidha Mwenge utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Ifulifu; kuzindua klabu ya wapinga rushwa katika Shule ya Sekondari ya Busambara; kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Bugoji/Kaburabura/Kanderema na kufanya mkesha katika eneo la stendi ya Saragana.
Ratiba hiyo imeonyesha kuwa tarehe 03 Julai, 2022 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambapo makabidhiano yatafanyika katika uwanja wa Kijiji cha Nyakisiwa na baadaye kukagua ujenzi wa tanki la maji eneo la Nyamikoma (Pida); kuzindua mradi wa vyumba vitatu vya madarasa na klabu ya wapinga rushwa na kukagua shughuli za klabu ya wapinga dawa za kulevya katika eneo la Kiabakari Sekondari; kuzindua zahanati ya Mmazami na kukagua mradi wa mapambano dhidi ya malaria.
Mwenge pia utaweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Butuguri; kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Butiama; kuzindua barabara ya Butiama- Rwamkoma; utawasha Mwenge wa Mwitongo, kuzuru kaburi la Baba wa Taifa na kusalimia familia ya Baba wa Taif ana baadaye kufanya mkesha katika uwanja wa Shule ya Msingi Nyamisisye.
Tarehe 04 Juni, 2022 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo makabidhiano yatafanyika katika eneo la Komongwe- Nyamuswa na baadaye kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu Shule ya Msingi Nyamuswa B; kuzindua mradi wa maji Bukama na kupanda miti katika eneo hilo.
Aidha Mwenge utazindua mradi wa ujenzi wa madarasa na klabu ya wapinga rushwa Shule ya Sekondari Chamriho; kukagua mradi wa ukarabati wa barabara na ujenzi wa makaravati katika barabara ya Kyandege- Tangirima; kutembelea mradi wa vijana wa ufugaji na kilimo katika eneo la Maliwanda; kuweka jiwe la msingi katika mradi wa Kituo cha Afya Hunyari na kufanya mkesha katika uwanja wa stendi ya Nyamswa.
Hatimaye tarehe 06 Julai, 2022 Mwenge utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na mapokezi yatafanyika katika eneo la Kisangwa na baadaye kuzindua kiwanda cha kuchakata mpunga eneo la Sazira; kuzindua mradi wa ujenzi wa madarasa na ofisi katika Shule ya Sekondari ya Bunda; kutembelea kikundi cha vijana cha African Top Shine katika eneo la Kabarimu.
Aidha mwenge pia utazindua mradi wa maji wa RUWASA; kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Wariku; Shule ya Sekondari ya Nyamakokoto; ujenzi wa daraja la TARURA na mkesha wa Mwenge utafanyika katika eneo la Stendi Mpya.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa kwa Mkoa wa Simiyu kuendelea na mbio zake tarehe 06 Julai, 2022 na makabidhiano yatafanyika katika Shule ya Sekondari ya Antony Mtaka.
Ratiba hiyo pia imeonyesha kuwa katika maeneo ya mkesha shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwa ni pamoja na kusoma risala ya utii; upimaji wa UKIMWI na Malaria; uchangiaji wa damu kwa hiari; burudani zitakuwepo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa