Mkoa wa Mara umejipanga kuongeza idadi ya watu wanaonufaika na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa) katika kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma.
Hayo yameelezwa leo tarehe 29 Julai 2021 katika kikao kazi cha wadau wa CHF iliyoboreshwa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara iliyopo katika Manispaa ya Musoma.
Wakizungumza katika kikao hicho, wajumbe wa kikao hicho wamesema kuna tatizo katika kuhamasisha watu wajiunge na CHF iliyoboreshwa kutokana na sababu mbalimbali ambazo pia zinawakwamisha waliojiunga kuendelea kulipia kupitia mfumo huo wa matibabu.
Maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuboresha huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya, kufunga mifumo ya malipo ya serikali (GOTHOMIS) katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona faida ya kutumia CHF iliyoboreshwa.
“Katika kutoa elimu tutawashirikisha viongozi wa kisiasa na serikali na kutumia mifumo ya kuwafikia wananchi kupitia viongozi wao wa serikali za vijiji na mitaa ili waweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi” walisema wajumbe hao
Maazimio mengine ni kuanzisha madawati ya CHF iliyoboreshwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kutoa elimu kwa wananchi; kuongeza ushirikiano na maafisa wa sekta nyingine ngazi ya Mkoa wenye watu hadi kwenye vijiji na kata ili waweze kusaidia kutoa elimu.
Akizungumza katika kikao hicho Mratibu wa CHF Mkoa wa Mara Bi. Elizabeth Mahinya ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa unawatu waliojiunga na CHF iliyoboreshwa 11,192 hata hivyo kati yao watu 3,861 kadi zao zimeisha muda wake wa matumizi na hawajalipia tena ili kuendelea kuzitumia.
“Kwa sasa kumekuwa na tatizo la mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na waliojiunga muda wa matumizi ukiisha hawalipii tena ili waendelee kuwepo katika mfumo huu” alisema Bi. Mahinya.
Bibi Mahinya amesema kuwa kufuatia tatizo hilo Mkoa ulichukua hatua mbalimbali ambazo kwa sasa zimeanza kuzaa matunda na kuongeza idadi ya watu wanaojiunga na mfuko huo.
Ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambayo awali ilikuwa chini katika uandikishaji lakini baada ya kuwakumbusha uandikishaji umepanda na wananchi wananufaika na CHF iliyoboreshwa.
Kwa upande wake Afisa wa Taasisi ya Health Promotion and System Strengthening (HPSS) katika Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara, Bwana Andrea Wilson Katamiti ameeleza kuwa CHF iliyoboreshwa inaweza kuwasaidia sana wananchi katika kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
“Familia yenye watu sita inalipia shilingi 30,000 na inatibiwa kwa kipindi cha mwaka mmzima katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya” ameeleza Bwana Katamiti.
Bwana Katamiti ameeleza kuwa vituo vya kutolea huduma za afya vinahitaji elimu zaidi ili viweze kuona kuwa vikiboresha huduma na kuvutia wanachama wengi wa CHF iliyoboreshwa vinaweza kupata fedha nyingi.
CHF kama Mfuko wa Afya ya Jamii ni mpango wa hiari wa uchangiaji wa huduma za matibabu kwa ajili ya familia na kaya zenye kipato cha chini na zilizokwenye mfumo usiokuwa rasmi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa