Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unajipanga kuanza kunufaika zaidi na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika Mkoa wa Mara.
Hayo yameelezwa leo katika hafla ya makabidhiano ya ofisi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Eng. Robert Gabriel Luhumbi na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi yaliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Maafisa wa TANAPA (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa) walikuja leo ofisini kwangu wameniambia kuwa Hifadhi yote ya Taifa ya Serengeti ipo katika Mkoa wa Mara, pale ambapo Hifadhi ya Serengeti inapoishia ndio mpaka wa Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha, jambo ambalo limenishangaza sana” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa awali alidhania asilimia 70 ya ardhi ya Serengeti ndio ipo katika Mkoa wa Mara jambo ambalo ameelezwa na Mhifadhi Mkuu wa TANAPA Kanda ya Magharibi kuwa sio sahihi, eneo lote la hifadhi lipo katika Mkoa wa Mara.
Ameeleza kuwa watu wanaifungamanisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Arusha kwa sababu ya miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Arusha na miundombinu mingine ambapo watalii wengi wamekuwa wakiitumia kwa ajili ya kuja Serengeti na kufanya wanufaika wakuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa ni Arusha.
“Tunaenda kufanyakazi kubwa sana ya kuutangaza Mkoa wa Mara ndani na nje ya nchi ili wawekezaji waweze kuelewa mambo mazuri na fursa za uwekezaji zilizomo katika Mkoa wa Mara ili wananchi wa Mara waweze kuonja matunda ya fursa zilizopo katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa baada ya uwanja wa ndege wa Musoma unaoendelea kupanuliwa kukamilika, ndege kubwa za abiria zitarudi Musoma jambo ambalo litarahisisha watalii wengi kuingia Serengeti wakitokea Musoma kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unautajiri mkubwa sana wa madini mbalimbali, Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni urithi wa dunia katika utalii.
“Tunataka uchumi na uwekezaji utakaofanyika Mkoa wa Mara ufanane na wingi wa utajiri wa asili uliopo, hili ndilo jambo mimi na wenzangu tunaenda kulifanyia kazi kwa haraka sana ili wananchi waweze kufaidi matunda ya utajiri uliopo katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa umejikita zaidi katika kuhamasisha ujenzi wa mahoteli ya kisasa katika Mji wa Bunda na Mugumu ambayo ni malango makuu ya kuingilia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ametoa mfano wakati wa Serengeti Marathon ambayo hufanyika mwezi Novemba ya kila mwaka, watu wengi wanaohudhuria wanakosa vyumba vya kulala na kulazimika kulala mbali na Mji wa Bunda hivyo ameeleza kuwa panahitajika uwekezaji mkubwa.
Mheshimiwa Hapi amewaomba wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Mkoa ili Mkoa uweze kupiga hatua katika maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Eng. Robert Gabriel Luhumbi amemkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mara kuendelea kazi mbalimbali ambazo yeye na watangulizi wake walikuwa wamezianza.
Mheshimiwa Hapi amehamishiwa Mara kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko tarehe 11 Juni 2021.
Makabidhiano hayo pia yalihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi wa Wilaya, Halmashauri, viongozi wa dini, watendaji wa Sekretariati ya Mkoa wa Mara, wakuu wa taasisi za umma na waandishi wa habari.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa