Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameeleza kuwa uongozi wa Mkoa wa Mara umejipanga kuiboresha Timu ya Biashara United ili iweze kufanya vizuri katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo leo tarehe 29 Septemba 2021 wakati alipokuwa anakabidhi shilingi milioni 10 alizowaahidi wachezaji wa Timu ya Biashara United baada ya kutoka sare katika mchezo wao na Timu ya Simba ya Jijini Dar es Salaam makabidhiano yaliyofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa tunafanya mazungumzo na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuidhamini timu ya Biashara United kwa udhamini mkubwa zaidi wenye thamani ya zaidi ya bilioni moja katika msimu huu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kutokana na udhamini huo, Biashara United itakuwa na uhakika wa fedha za kuendeshea timu hiyo ikiwa ni pamoja na mishahara ya wachezaji na usafiri wa timu katika kushiriki mechi mbalimbali.
Mheshimiwa Hapi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Timu ya Biashara United ameipongeza timu hiyo kwa mchezo mzuri waliouonyesha na kuiwezesha timu kupata sare katika mechi hiyo waliyocheza na Timu ya Simba.
Aidha amewapongeza wachezaji kwa mafanikio waliyoyapata katika msimu uliopita na mechi mbili walizocheza nje ya nchi ambazo Timu ya Biashara United ilifanya na amewataka wachezaji kujitoa kuinyanyua timu hiyo iweze kupata ubingwa msimu huu ili iwe rahisi kupata udhamini tena miaka inayofuata.
Mheshimiwa Hapi amempongeza golikipa wa Timu ya Biashara United Bwana Ssetuba James Cleo kwa jitihada kubwa alizozifanya katika mechi hiyo ikiwa ni pamoja na kudaka mpira wa penati iliyopigwa na mchezaji wa Timu ya Simba.
Ameeleza kuwa kabla ya mechi hiyo alitoa ahadi ya yeye pamoja na wapenzi wa Biashara United wangetoa shilingi milioni 15 kama Biashara United ingekuwa mshindi katika mechi hiyo na milioni 10 kama wangetoka sare, jambo ambalo wachezaji wamelitimiza.
“Katika fedha nilizokabidhi leo wachezaji wote 31 wa Biashara United watapata shilingi laki tatu kila mmoja na fedha inayobakia itagawiwa kwa benchi la ufundi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa michezo inaunganisha watu na uongozi wa Mkoa wa Mara utaendelea kuwa pamoja na Biashara United ili iweze kufanya vizuri zaidi na kuendelea kuutangaza Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Timu ya Biashara United Bwana Selemani Mataso amemshukuru Mheshimiwa Hapi kwa kutekeleza ahadi yake ambayo imewapa hamasa na kuwajengea ari wachezaji wa timu hiyo.
“Mwaka huu tumeisajiri timu vizuri sana tunasubiria vibali tu vya baadhi ya wachezaji wetu, vikipatikana tunaweza kufanya vizuri zaidi, Ubingwa unakuja Mkoa wa Mara msimu huu” alisema Bwana Mataso.
Bwana Mataso ameeleza kuwa kwa sasa vipaumbele vyao ni kuona timu inawalipa wachezaji stahiki zao kwa wakati na kumpongeza mwalimu wa Timu hiyo kwa kazi kubwa anayoifanya kuwaimarisha wachezaji wake katika mazoezi.
Mechi ya Simba na Biashara United ilifanyika tarehe 28 Septemba 2021 katika Uwanja wa Karume uliopo katika Manispaa ya Musoma ambapo timu zilitoka sare ya bila kufungana pamoja na Timu ya Simba kupata penati katika mchezo huo.
Katika msimu uliopita wa 2021/2022 Timu Biashara United ilidhaminiwa na Mgodi wa North Mara kwa shilingi milioni 350 na Kiwanda cha Jamakaya cha Shinyanga kwa shilingi milioni 100 pamoja na wadhamini wengine ambao walikuwa wanadhamini baadhi ya mahitaji ya timu hiyo na ilifanikiwa kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi ya Tanzania Bara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa