Mkoa wa Mara unampango wa kuanza kulima zao la mkonge kama zao kuu la biashara kwa wakazi wa Mkoa wa Mara katika msimu huu wa kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 19 Februari 2021, Mkuu Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amesema kwa kuanzia Mkoa umeazimia kulima ekari 6,000 katika halmashauri za wilaya za Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, na Serengeti.
“ Kwa sasa tayari halmashauri hizi zimetenga maeneo ya ekari 10 kila mmoja kwa ajili ya kuanzisha vitalu vya miche ya mkonge na kisha kuwagawia wakulima watakaolima mkonge katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa ili kulima ekari hizi 6,000 Mkoa umeaagiza miche 10,400,000 kutoka Tanga.
Aidha Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa Mkoa pia kwa kushirikiana na Pamba Mara Cooperative Limited unampango wa kuchukua mkopo wa shilingi bilioni 2.5 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kufadhili shughuli za uendelezaji wa zao la Mkonge katika Mkoa wa Mara.
“Fedha hizi pamoja na mambo mengine zitatumika kulima shamba, kununua matrakta matatu, kufanya utafiti wa udongo, kufadhili gharama za mafunzo ya maafisa ughani 40 ambayo yatatolewa na Chuo Kikuu cha Mwalimu J. K. Nyerere, Butiama” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha mheshimiwa Malima ameeleza kuwa katika malengo ya muda mrefu, Mkoa wa Mara unampango wa kulima ekari 30,000 za zao la mkonge katika halmashauri hizo sita.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, waandishi wa habari na wadau wengine kuhamasisha kilimo cha zao la mkonge katika halmashauri zao ili kuweza kuinua hali ya uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima Mkonge sio zao geni katika Mkoa wa Mara liliwahi kulimwa miaka ya zamani katika baadhi ya maeneo hata hivyo baadaye liliachwa kutokana na kukosa usimamizi na soko la uhakika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa