Mkoa wa Mara umeanza kutoa mafunzo ya utambuzi na namna ya kuwahudumia wagonjwa wa Seli Mundu kwa wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere na Chuo cha Matabibu Musoma ikiwa na lengo la kuuwezesha Mkoa wa Mara kukabiliana na tatizo la seli mundu.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyotolewa na taasisi ya Tanzania Sickle Cell Disease Alliance (TSDA) Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu amesema kwa wataalamu hao kupewa mafunzo kutawawezesha kutoa mafunzo kwa wataalamu wengine na wanafunzi wanaosoma katika Chuo cha Matabibu na baadaye watatumika kama walimu kwa ajili ya kuwafundisha wataalamu wengine.
“Hawa tutawatumia baadaye kama walimu ili waweze kutoa mafunzo haya kwa wataalamu wa ngazi za Halmashauri, vituo vya afya na zahanati ili kuwatambua na kuwahudumia wagonjwa wa selimu mundu katika maeneo yao” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu amesema kuwa awali ugonjwa wa Selimundu ulikuwa ni kati ya magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele japokuwa yamekuwa ni mzigo mkubwa sana kwa wazazi na walezi wa wagonjwa wenye tatizo hilo na hususan kama hatua hazikuchukuliwa mapema.
Dkt. Masatu amesema Mkoa wa Mara unao wagonjwa wengi sana wenye tatizo hilo na hususan katika Wilaya za Rorya, Musoma na Serengeti na kuongeza kuwa mafunzo hayo kwa wataalamu yatawasaidia wataalamu hao wanapowahaudumia wagonjwa wa selimundu ikiwa ni pamoja na kuwapatia taarifa sahihi za namna ya kutibu na kupima.
“Kwa Tanzania kila mwaka watoto milioni 14 wanazaliwa na ugonjwa huo na wengi wao wakiwa wanatoka katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Mara” amesema Dkt. Masatu na kuiomba taasisi ya TSDA kuusaidia Mkoa katika kutoa vifaa na vitendanishi ili waweze kuwapima watoto.
Akizungumza katika mafunzo haya, Mwenyekiti wa TSDA Dkt. Elisha Osati amesema lengo la mafunzo haya ya siku mbili ni kuuvunja mduara na kuwapima vijana kabla ya kuanzisha familia ili wajue hali zao kuhusiana na ugonjwa huo ili waweze kuanzisha familia ambazo au hazina mgonjwa au zinafahamu namna ya kumtunza mgonjwa huo ili kupunguza athari za ugonjwa.
Dkt. Osati amesema kuwa Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye wagonjwa wengi zaidi ambapo asilimia 22 ya watu wanavinasaba vya ugonjwa huo japokuwa wengine wanaweza kuwa hawajui na hawaumwi kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dkt. Osati, wagonjwa wa Seli Mundu wanaweza kuishi muda mrefu kama wakipimwa na kujulikana mapema na kupatiwa dawa za kuufubaza kutokana na teknolojia mbalimbali zilizopo na kwa sasa kuna uwezekano wa kutibiwa na kupona kabisa japokuwa matibabu ni gharama kubwa.
Dkt. Osati ambaye pia ni Daktari wa Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amesema kuwa ni matumaini yao kuwa wataalamu wlaiojengewa uwezo waende kuwaelimisha wataalamu wanaotoa huduma katika Hospitali za Halmashauri, vituo vya afya na zahanati katika Mkoa wa Mara.
Dkt. Osati amesema ni matumaini ya TSDA kuwa Mkoa wa Mara uwe wa mfano katika kuchukua hatua na kupambana na tatizo la Seli Mundu ikizingatiwa kuwa tatizo la ugonjwa wa Seli Mundu ni kubwa sana kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wao Mkuu wa Chuo cha Matabibu Musoma na Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wameshukuru kwa mafunzo hayo na kuahidi kuwa wataalamu wao watayatumia mafunzo hayo katika kuwahudumia wagonjwa na kuwafundisha wataalamu wengine.
Aidha, wamewaomba wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambao wanawawezesha katika mafunzo hayo, kuendelea kutoa elimu kwa wataalamu wa afya ili waweze kuwahudumia wagonjwa wa Selimundu na hususan wanapopata matatizo mengine ya kiafya.
Kwa upande wake, Bibi Neema Mohammed ambaye ni shujaa wa Selimundu na mfanyakazi wa TSDA amesema aligundulika na ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 10 na tatizo kubwa analolipata ni maumivu kwenye viungo, upungufu wa damu na hivyo kulazimika kuongezewa damu mara kwa mara.
Bibi Mohammed amesema baadhi ya dalili ambazo ni rahisi kutambulika ni pamoja na kupata njano kwenye macho, viganja, kuwa na joto kali na mgonjwa kusikia baridi kali.
Bibi Mohammed amesema kwa sasa vipimo vya ugonjwa wa selimundu vipo na matibabu yapo japokuwa gharama za matibabu zipo juu sana na hivyo sio rahisi sana kwa wananchi wa kawaida kuweza kuyamudu.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika Chuo cha Matabibu Musoma na kuwahusisha wadau mbalimbali ikiwemo taasisi ya TSDA na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa