MARA YAJADILI MPANGO MKAKATI WA CHAKULA SHULENI
Wadau wa elimu wa Mkoa wa Mara leo tarehe 23 Septemba 2020 wamejadili rasimu ya Mpango Mkakati wa Chakula na Lishe Shuleni Mkoa wa Mara wenye lengo la kuboresha taaluma, kuinua ufaulu na afya za wanafunzi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa kujadili rasimu ya mpango huo, mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mheshimiwa Dkt. Vincent Anney Naano amewahimiza wajumbe kuchangia rasimu hiyo ili kupata mkakati mzuri.
“Mara ni mkoa wa kwanza kuandaa Mpango Mkakati wa Chakula na Lishe Shuleni, kwa hiyo mpango huu utatumika na mikoa mingine kama rejea watakapokuwa wanaandaa mipango yao, hivyo ni vizuri tuutendee haki kwa kuchangia maoni yetu na baadae wataalamu watayafanyia kazi” alisema Mheshimiwa Naano.
Mheshimiwa Naano ameeleza kuwa Mpango Mkakati wa Chakula na Lishe Shuleni unatokana na kikao cha wadau cha kujadili changamoto za elimu katika Mkoa wa Mara kilichafanyika tarehe 23 Februari 2020 ambapo uliazimia kuanzisha mpango wa chakula mashuleni.
“Katika mkutano ule, tafiti mbalimbali za changamoto za elimu zilizofanywa katika Mkoa wa Mara zilionyesha kuwa chakula kilikuwa ni moja ya vitu muhimu vya kupewa kipaumbele katika uboreshaji wa elimu katika Mkoa wa Mara”.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karoline Mthapula amesema kuwa chakula mashuleni kitaboresha afya na lishe za wanafunzi, itasaidia kuongeza mahudhurio, uandikishaji na usikivu wa wanafunzi darasani.
“Kwa zile shule ambazo chakula kinatolewa shuleni, wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri ukilinganisha na shule ambazo hazina chakula kabisa” alisema Bibi Mthapula.
Aidha amelipongeza Shirika la Project Concern International (PCI) Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Mkoa wa Mara hususan katika utoaji wa chakula katika baadhi ya shule zinazofikiwa na mradi wa Chakula Shuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi wa PCI Tanzania Bi. Amina Mgeni amesema shirika la PCI limekuwa likifanyakazi na Halmashauri nne za Mkoa wa Mara ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Halmashauri ya Musoma Vijijini na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Bi. Mgeni ameeleza kuwa mpango mkakati huu unalenga kutoa mwongozo wa uzalishaji na uchangiaji wa chakula kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mkutano wa kujadili rasimu ya Mpango Mkakati wa Chakula na Lishe Shuleni katika Mkoa wa Mara umehudhuriwa na wataalamu na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wanafunzi, walimu na watumishi wa PCI na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa