Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, leo ameongoza warsha ya wadau kutambulisha mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknlojia (MJNUAT) baada ya kupokea mkopo wa masharti nafuu shilingi bilioni 102.3 kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumza katika kikao hicho Mheshimiwa Mzee amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na kuanzishwa kwa Chuo hicho cha kwanza cha umma katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Mimi ninaamini Chuo hiki kitachagiza maendeleo ya Mkoa wa Mara, wito wangu ni wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za kuanzishwa kwa Chuo hiki katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewataka watendaji na viongozi wote watakaohusika katika ujenzi huo kuzingatia uadilifu, weredi na mradi kukamilika kwa wakati ili manufaa ya mradi huu yaonekane mapema.
Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi katika maeneo mbalimbali kuwaelimisha wananchi kuhusiana na fursa zilizopo kutokana na kuanzishwa kwa Chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa nafasi za mafunzo ya elimu ya juu ili wananchi nao waweze kuchukua hatua za maksudi kuboresha shughuli mbalimbali.
Ameahidi kuwasimamia watendaji na viongozi wote wa Mkoa wa Mara kutatua changamoto zote zinazoweza kukkwamisha utekelezaji wa mradi huo katika hatua mbalimbali.
Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lesakit Mellau ameeleza kuwa lengo la Serikali kuanzisha Chuo cha MJNUAT hicho ni kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Makao Makuu ya Chuo hicho yatakuwa katika Wilaya ya Butiama.
Prof. Mellau ameeleza kuwa mpaka sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari amemteua Mheshimiwa Peter Pinda, Waziri Mkuu Msaatafu kuwa Mkuu wa Chuo hicho na Katibu Mkuu Kiongozi Mtaafu Bwana Philemon Luhanjo kuwa mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho.
Prof. Mellau ameeleza kuwa katika mradi wa ujenzi unaoanza sasa, ujenzi utafanyika katika maeneo mawili, Kampasi kuu ambayo inatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Butiama na Kampasi ya Tabora ambayo inatarajiwa kujengwa katika Mkoa wa Tabora.
“Hii inatokana na maamuzi ya Serikali ya kuvitaka Vyuo vikuu vya Umma kuanzisha Kampasi katika mikoa mbalimbali na kwa Chuo chetu Kampasi itajengwa Tabora ambayo itakuwa na majengo 7 kati ya majengo 28 yanayojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia” alisema Prof. Mellau.
Prof. Mellau ameeleza kuwa ujenzi wa awamu hii ukikamilika, Chuo kitaweza kudahili wanafunzi 6,000 na kitakuwa na watumishi wa Chuo zaidi ya 1,000 ambalo amesema litakuwa ni ongezeko kubwa sana la watu katika Mkoa wa Mara.
Prof. Mellau ameeleza kuwa tayari Chuo hicho kimeandika miradi mbalimbali na ikifadhiliwa yote Chuo kitakuwa na miundombinu ya kutosha ili kudahili wanafunzi 15,000 katika Kampasi mbalimbali za Mkoa wa Mara na Tabora.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Fedha, Mipango na Utawala Prof. Msafiri Jackson ameeleza kuwa ujenzi huo utahusisha ndaki ya Kilimo, Shule ya Uhandisi na Teknolojia, Shule ya Uhandisi na Teknolojia Nishati na Madini, Shule Kuu ya Tehama na Biashara, jengo la Utawala, Maktaba, mabwalo mawili ya chakula, viwanja vya michezo, barabara na mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,220.
Prof. Jackson ameeleza kuwa mradi huo ni wa miaka mitano ukijumuisha ujenzi wa miundombinu, mafunzo kwa watumishi na tafiti mbalimbali na kuongeza kuwa ujenzi umeanza, mafunzo kwa watumishi yanaendelea na tafiti zimeanza tarari zimeanza kufanyika.
“Changamoto kubwa tutakayokutana nayo ni uhaba wa mabweni ya wanafunzi na nyumba za watumishi, kituo cha polisi, kituo cha kutolea huduma za afya, barabara, hoteli na kadhalika.
Kikao kilihudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Kamatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na taasisi za serikali.
Wengine ni wazee mashuhuri, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa kimila, wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa