Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Tarime kulingana na muda uliopo katika mkataba wao.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 23 Julai 2021 wakati Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi katika Mkoa wa Mara ilipotembelea mradi huo.
“Huu mradi umechelewa sana bila sababu za msingi, sasa nataka tarehe 28 Septemba 2021 mradi huu uwe umekamilika na uanze kutumika na hakutakuwa na nyongeza tena ya muda wa utekelezaji wa mradi huu” ameagiza Mheshimiwa Hapi.
Ameitaka TBA baada ya siku tatu kufunga taa katika eneo hilo na kuanza kutekeleza mradi huo usiku na mchana ili uweze kukamilika kwa wakati na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Aidha mamemtaka msimamizi wa mradi huo kusafisha mazingira ya maradi huo “Na sitaki kukuta site chafu namna hii nikija tena” alisema Mheshimiwa Hapi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye amesema kuwa TBA wanatabia ya kuchelewesha miradi
“Ningekuwa mimi ndio ninatoa tenda nisingekuwa ninawapatia tenda TBA, hawa wakishachukua pesa wanapotea na wakisikia tunakuja kukagua wanarudi kwenye mradi” alisema Mheshimiwa Kiboye.
Mheshimiwa Kiboye ameeleza kuwa mradi huo wameukataa kwa sababu unatekelezwa kwa muda mrefu mmno bila sababu za msingi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo kwa upande wa TBA Mhandisi Mohammed Mohammed ameeleza kuwa mkataba wa ujenzi wa jengo hilo ni bilioni 3.1 na kati ya hizo TBA tayari wameshalipwa shilingi bilioni 2.1.
“Kazi zinazoendelea katika eneo hili ni ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya kujenga kuta za jengo hili na kwa mujibu wa mkataba tunatarajia kukamilisha ifikapo tarehe 28 Septemba 2021”alisema Mhandisi Mohammed.
Ameeleza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na baadaye ulisimamishwa na serikali na kuanza tena baada ya muda.
Kamati ya Siasa ikiwa katika Wilaya ya Tarime ilitembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mradi wa jengo la ofisi za Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa