Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuimarisha sekta ya afya na kuutendea haki Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Malima ametoa shukrani hizo leo tarehe 13 Mei 2020 wakati wa kupokea gari ya kubebea wagonjwa ambayo imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Amina Makilagi.
“Hizi gari zilikuwa 16 tu kwa nchi nzima lakini sisi Mkoa wa Mara tumepata gari moja ambayo imepangiwa kutoa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama, tunashukuru sana” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuwapangia madaktari 62 kuja kufanya kazi katika Mkoa wa Mara katika mgao wa madaktari wapya 1,000 walioajiriwa hivi karibuni.
“Kati ya madaktari hawa 62, madakatari 23 ni kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara na wengine waliobakia ni kwa ajili vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za halmashauri” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa huu ni uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya afya na kuwataka watumishi wa afya kuhakikisha wanalitunza gari hilo ili liweze kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Mara amepokea na kukabidhi pikipiki 16 zilizotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Mara.
Akikabidhi pikipiki hizo Mheshimiwa Malima amewataka Maafisa Tarafa kuzitumia kwa makusudi yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mheshimiwa Amina Makilagi amemshukuru Rais na serikali ya awamu ya tano kwa ujumla kwa jinsi wanavyoujali Mkoa wa Mara.
“Tunashukuru kwa kuweza kutoa fedha za kujenga vituo vya afya na hospitali za wilaya pamoja na kumalizia hospitali ya rufaa” alisema Mheshimiwa Makilagi.
Hata hivyo bado tunaendelea kufuatilia maombi ya magari zaidi ya kubebea wagonjwa hususan kwa ajili ya Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga ameeleza kuwa msaada huo wa gari ya wagonjwa imefika wakati muafaka ambapo uhitaji ni mkubwa sana.
“Kwa sasa Mkoa wa Mara ulikuwa na magari ya wagonjwa 29 na baada ya kuongezewa moja sasa tuna magari 30 ya kubebea wagonjwa” alisema Dkt. Tinuga.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki ameishukuru serikali kwa kutoa pikipiki 16 kwa ajili ya maafisa tarafa wa Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa Mkoa wa Mara una tarafa 20 na kati ya hizo tarafa 16 zimepatiwa pikipiki mpya na wanakabidhiwa leo” alisema Mama Mthapula.
Kwa upande wake Afisa Tarafa wa Ikolongo katika Wilaya ya Serengeti Bwana Erick Evaristo Ngole aliyepokea pikipiki kwa niaba ya wenzake, ameishukuru serikali kwa kutoa pikipiki hizo ambazo zitawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa