Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amekagua Kituo cha Forodha Sirari leo tarehe 19 Mei 2020 na kusisitiza kuhusu maagizo aliyoyatoa awali kuhusiana na hatua mpya za kudhibiti ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona yaani COVID 19.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa katika maelekezo aliyoyatoa magari na abiria wote kutoka katika nchi ya Kenya hawataruhusiwa kuingia Tanzania kwa sababu ya kudhibiti maambikizi ya Corona katika nchi hizi mbili.
“Kama nilivyoelekeza awali, maagizo yangu hayajabadilika, utaratibu wetu utaendelea kama kawaida hadi hapo nitakapoelekeza vinginevyo” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima alisema kuwa ziara hiyo imekuja baada ya kupokea taarifa kuwa kuna magari ya Kenya matano yaliyoingia nchini kupitia mpaka huo kinyume na maagizo yake jambo ambalo amehakikisha kuwa halikuwa sahihi.
Msheshimiwa Malima amewakumbusha maafisa wa mpaka huo kuwa magari yote kutoka nchi ya Kenya yanaishia mpakani na anayehitaji mzigo uliobebwa ataufuata hapo ili kudhibiti maambukizi ya Corona.
Ameeleza kuwa tangu ugonjwa wa corona umeanza, Mkoa wote wa Mara umekuwa na wagonjwa watano ambao wote walitokea katika Mkoa wa Dar es Salaam na kati ya hao mmoja alifariki lakini wengine wanne wamepona na wanaendelea kufanya shughuli zao.
“Ninashangazwa majirani zetu wanaposema sisi ndio tunawaletea ugonjwa wa Corona jambo ambalo sio sahihi” alisema Malima.
Aidha alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya hatua zinazochukuliwa na nchi ya Kenya hususan kutangaza watanzania wenye Corona na kuamua kufunga mpaka jambo ambalo amesema huenda halijatazamwa vizuri.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Malima aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karolina Mthapula, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Eng. Mtemi Msafiri na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa