MARA YAENDELEZA UBABE UMITASHUMTA
Mkoa wa Mara umeendeleza ushindi katika Mashindano ya 26 ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mwaka 2022 baada ya kuibuka mshindi wa pili wa jumla kwa kupata pointi 125.2.
Akizungumza baada ya kupokea matokeo hayo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Benjamin Oganga ameeleza kuwa katika mashindano hayo, Mkoa wa Mara umefanikiwa kushinda jumla ya makombe manne.
Bwana Oganga ameeleza kuwa mikoa mingine iliyofanya vizuri katika UMITASHUMTA ni Mwanza ambao umeongoza kitaifa kwa kupata pointi 160.3; na kufuatiwa na Mkoa wa Mara wenye pointi 125.2, Mkoa wa Tabora wenye pointi 115.7, Mkoa wa Geita (109.7) na Mkoa wa Dar es Salaam ambao umepata jumla ya pointi (109.5).
Bwana Oganga ameeleza kuwa katika mashindano hayo Mikoa ambayo haikufanya vizuri sana ni pamoja na Unguja yenye pointi 24.2, Pemba yenye pointi 28.4, Mkoa wa Ruvuma wenye pointi 39.7 na Mkoa wa Katavi ambao umepata pointi 45.9.
Bwana Oganga ameeleza kuwa katika mashindano hayo, Mkoa wa Mara umefanya vizuri katika Nidhamu na Usafi ambapo kwa wasichana wamekuwa washindi wa kwanza wakati kwa wavulana wamekuwa washindi wapili.
Mashindano ya UMITASHUMTA ilifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde na kufungwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul.
Akifunga mashindano hayo katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, Mheshimiwa Gekul ameitaka Mikoa na Halmashauri zote nchini kusimamia ushiriki wa shule za binafsi katika mashindano ya michezo kwa wanafunzi.
Mwaka 2021 Mkoa wa Mara ulikuwa mshindi wa kwanza wa UMITASHUMTA Kitaifa nafasi ambayo imechukuliwa na Mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa