Serikali ya Mkoa wa Mara imeimarisha mpaka wa Tanzania na Kenya katika vijiji 14 vilivyopo katika wilaya za Tarime na Rorya ili kudhibiti maambikizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza hayo baada ya kupokea msaada kutoka katika Hoteli ya Kitalii ya Grumeti ya sare na buti za jeshi la akiba pea 100 na vipama joto 15 ili kuunga jitihada za Mkoa katika kupambana na Corona.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara katika vikao vyake na baada ya ziara waliofanya ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika Wilaya za Tarime na Rorya iliamua kuweka Jeshi la Akiba ili liweze kusaidia katika kudhibiti mapambano ya watu wanaoingia Tanzania kupitia vichororo vilivyopo mpakani” alisema Mheshimiwa Malima.
Mhehsimiwa Malima ameeleza kuwa pamoja na askari hao wa Jeshi la Akiba, Mkoa pia umefufua magari machakavu 14 ili yaweze kutumika katika mpango huu maalum wa kuzuia uingiaji holela wa watu kutoka Kenya pasipo kupita katika mipaka rasmi ya nchi.
Alisema kuwa mpaka huo una urefu wa zaidi ya mita 130 na una vijiji 14 ambavyo vyote vina sehemu mbili, sehemu ya Tanzania na sehemu ya Kenya katika kila kijiji. Aidha alisema kuna vichochoro vingi sana na wahalifu na watu wasiofuata sheria wanavuka mpaka kwa kutumia magari binafsi, pikipiki na baiskeli kupitia vichochoro hivyo.
“Kwa kuimarisha mpaka huu, sio tu tutadhibiti Corona lakini pia tutadhibiti magendo na vitendo vyote visivyofaa katika mpaka huo” alisema Malima.
Msaada huu umekuja wakati muafaka, hususan wakati huu ambapo tunapambana na virusi vya Corona” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Hoteli ya Grumeti Bwana David Nicholaus Mwakipesile ameeleza kuwa lengo la msaada huo ni kuunga mkono juhudi za mkoa katika kupambana na virusi vya Corona.
“Sisi kama Grumeti tunaunga mkono juhudi kubwa inayofanya na serikali ya Mkoa na tunaamini Mkoa wa Mara ukiwa salama, na sisi tutakuwa salama na tutapata wateja” alisema Bwana Mwakipesile.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mara Dkt. Florian Tinuga amewashukuru sana Grumeti kwa msaada huo na utausaidia sana Mkoa kudhibiti maambukizi ya Corona.
“Ninawashukuru sana kwa msaada huu na msaada mwingine wa kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Serengeti” alisema Dkt. Tinuga.
Katika mpango huo, Jeshi la akiba litaungana na vikosi vya uhamiaji, polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kudhibiti mpaka huo katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapambana na kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa corona.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa