Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka wakandarasi waliopewa zabuni za kujenga barabara mbalimbali katika Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao kikamilifu kwa mujibu wa mikataba yao.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mara kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Uwekezaji uliomo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Hatutakubali, hatutawavumilia wala hatutawafumbia macho wakandarasi wababaishaji ambao wanalipua kazi na kutokulipa wafanyakazi wao, wasiotekeleza kazi kwa haraka” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Mara walioko vijijini wanategemea sana barabara za TARURA na kutoa rai kuwa barabara zitakazofanyiwa kazi zilenge katika kuwasaidia wananchi kujenga uchumi wao na kuwaunganisha wananchi na huduma za kijamii.
Amezitaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kutoa mafunzo kwa wakandarasi wa Mkoa wa Mara ili kuwajengea uwezo waweze kutekeleza miradi kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Hapi amezitaka taasisi hizo wakati wa kutoa zabuni kwa wakandarasi kutoa kipaumbele kwa wakandarasi ambao wanauwezo, wasio na ubabaishaji katika kutekeleza miradi kwa mujibu wa mikataba yao.
“Hatutawapa kazi wakandarasi wa Mkoa wa Mara kwa kwa sababu tu ni wenzetu, tunawafahamu” alisema Mheshimiwa Hapi na kuwataka wakandarasi watekeleze miradi kwa viwango vinavyokubalika bila ubabaishaji.
Aidha amewataka Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Mara kuaajiri watu kutoka katika maeneo wanapofanyia kazi hususan zile kazi ambazo hazihitaji ujuzi maalum ili kutoa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Mara
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia miradi ya barabara inayotekelezwa katika maeneo yao na kuifuatilia kwa karibu kuweza kujiridhisha kuhusu hali halisi ya miradi hiyo.
Wakati huo huo, Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kimemchagua kwa kauli mmoja Mheshimiwa Jumanne Sagini, Mbunge wa Butiama, kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Sagini ambaye ni Katibu Mkuu na Katibu Tawala Mstaafu amechaguliwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kupendekeza jina lake na wajumbe wa kikao hicho kuridhia kwa kauli mmoja.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Meya na wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi wa serikali za mitaa, Kamati ya Usalama ya Mkoa, wasimamizi wa masuala ya usafiri na Sekretarieti ya Mkoa na wadau wa usafiri katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa