Mkoa wa Mara umedhamiria kuwa kinara wa biashara na uwekezaji kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mkoani humo. Hayo yameelezwa katika Mkutano wa Mashauriano kati ya serikali, wafanyabiashara na wawekezaji uliofanyika tarehe 24 Februari 2020 katika ukumbi wa Mwembeni, Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkuatano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Mara unajipanga kuweza kuongeza uzalishaji na tija ya shughuli mbalimbali zinazofanyika katika mkoa huu ikiwa ni pamoja na kilimo cha Kahawa na Pamba.
“Kwa muda mrefu Mara ni Mkoa ambao fursa zake na raslimali zake zilikuwa zimejificha na kunufaisha mikoa mingine. Kama Mkoa tumeamua kutangaza fursa na rasilimali mbalimbali zilizomo ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara zaidi.”
Akitoa mfano wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mazao yatokanayo na Ziwa Victoria na madini yaliyopo mkoani humo, ambavyo awali vilikuwa vinainufaisha mikoa na nchi jirani lakini vipo katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara, Bwana Boniface Ndengo amesema taasisi yao inalengo la kuufanya Mkoa wa Mara kuwa lango kuu la biashara kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. “Tumechukua jitihada za maksudi kuhakikisha tunawakuza wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Mara ili kuuwezesha Mkoa wetu uweze kukua kiuchumi”
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mheshimiwa Angela Kairuki, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya. Aidha ulihudhuriwa pia na maafisa mbalimbali wa serikali ikiwemo wawakilishi wa Makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa taasisi, wawakilishi wa wakuu wa taasisi na maafisa waandamizi wa serikali.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wote wa Mkoa wa Mara, wawakilishi kutoka katika vyama mbalimbali vya wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wakuu wa taasisi zote zilizomo katika Mkoa wa Mara. Katika Mkoa wa Mara mkutano huu umefadhiliwa na Kampuni ya Barrick kupitia mgodi wake wa North Mara, Benki ya NMB na Benki ya NBC.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa