Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam kighoma Ali Malima leo tarehe 18 Mei 2020 amekabidhiwa rasmi majengo mawili yaliyojengwa kwa ajili ya walinzi na watoa huduma wa Ikulu ndogo ya Musoma kwa ajili ya matumizi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa majengo hayo, Mheshimiwa Malima amemshukuru Katibu Tawala na Menejimenti ya Mkoa wa Mara kwa kusimamia ujenzi huo na kukamilisha kwa wakati.
“Mimi ninashukuru sana kwa mradi huu kutekelezwa vizuri na kwa wakati itatusaidia sana kama tutapata ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati huu” alisema Mheshimiwa Malima.
Hata hivyo Mheshimiwa Malima ameagiza kuanza mchakato wa kuomba fedha za ukarabati wa jengo la zamani ambalo kwa sasa halitumiki tena kutokana na uchakavu.
“Hili jengo japokuwa limechakaa sana lakini bado ni imara na ukarabati unaohitajika hapa ni mkubwa hususan paa ili liweze kufanana na mapaa ya majengo mengine hapa ndani” alisema Mheshimiwa Malima.
Mradi huu wa ukarabati ulihusisha ujenzi wa nyumba ya walinzi na nyumba moja ya mtumishi, ukarabati wa mfumo wa maji taka na maboresho katika mfumo wa umeme na ulitekelezwa kwa mfumo wa force account.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Karoline Mthapula ameeleza kuwa mradi huu umeghalimu kiasi cha shilingi 172,513,385.60 ambazo zilitolewa na serikali na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iliongeza fedha kidogo.
Bibi Mthapula ameeleza kuwa kati ya fedha hizo zote shilingi 94,528,536.40 zilinunua vifaa, ushauri wa kitaalamu uligharimu shilingi 8,778,900.00 wakati ufundi na baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa na mkandarasi vilikuwa na jumla ya shilingi 68,253,524.60.
Bibi Mthapula ameeleza kuwa ujenzi na ushauri wa kitaalamu katika mradi huu ulitolewa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).Amewashukuru wajumbe wote wa kamati za ujenzi zilizohusika kwa kazi kubwa walioifanya ili kufanikisha shughuli ya ujenzi.
“Ninawashukuru pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Mkurugenzi wa Wilaya ya Rorya, TANESCO, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kwa ushiriki wao katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huu” alisema Bibi Mthapula.
Bibi Mthapula ameahidi kuomba fedha katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa uzio na kukarabati jengo la Ikulu hiyo ili liweze kutumika kuwahudumia viongozi.
Kwa upande wake, Bwana Dominicus Lusasi, Afisa Tawala, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mradi huu ulipangwa kutekelezwa kwa muda wa miezi saba hata hivyo muda uliongezeka kutokana na changamoto mbalimbali.
Bwana Lusasi amezitaja changamoto kubwa kuwa ni pamoja na mfumo wa malipo ya serikali kusimama ilipofika Juni 2019 na hivyo kuchelewesha malipo ya mradi; kuchelewa kupatikana baadhi ya vifaa kwa wakati na maboresho ya michoro katika majengo wakati mradi unaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa