Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Mhandisi Faustine Tarai amewataka wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa Mkoa huu unakuwa katika kumi bora katika utekelezaji wa afua za lishe kitaifa kwa mwaka 2021.
Mhandisi Tarai ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ya Mkoa wa Mara kilichofanyika leo tarehe 18 Mei, 2021 katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninaomba wajumbe na wataalamu mliopo hapa tujitahidi ili tuweze kufika katika kumi bora kwa mwaka huu na baadaye tuboreshe zaidi hadi kufikia kuwa wa kwanza kitaifa” alisema Mhandisi Tarai.
Aidha amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa na wataalamu wengine kurekebisha mapungufu yanayojitokeza katika kadi alama lishe kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba 2021 ili wakati wa tathmini Mkoa uweze kupata nafasi nzuri zaidi.
Aidha amewataka wataalamu wa Lishe kutekeleza majukumu yao kikamilifu na pale wanapokwama kuomba msaada kwa watendaji wengine ili kuweza kuleta ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya lishe hususan kwa wajawazito na watoto.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Kaimu Katibu Tawala, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya Dkt. Florian Tinuga ameeleza kuwa katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mara umepiga hatua kutoka kuwa mwishoni hadi nafasi ya 17 kitaifa mwaka.
“Kama Mkoa tumedhamiria kuboresha utekelezaji katika upande wa lishe na tumefanikiwa sana kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa wataalamu mbalimbali na viongozi katika Mkoa wa Mara” alisema Dkt. Tinuga.
Viashiria vinavyopimwa ni pamoja na asilimia ya vikao vya Kamati ya Lishe katika ngazi za halmashauri, asilimia ya usimamizi shirikishi, asilimia ya kaguzi za chakula, asilimia ya wamama waliopewa ushauri wa ulishaji na wahudumu wa afya ngazi ya jamii na asilimia ya wamama waliopewa ushauri wa ulishaji na wahudumu wa afya vituoni.
Viashiria vingine ni asilimia ya watoto waliopatiwa matibabu ya utapiamlo; asilimia ya watoto waliopatiwa matone ya vitamin A; asilimia ya madini ya chuma kwa wamama wajawazito; fedha zilizotumika; fedha zilizotengwa na halmashauri.
Aidha katika kikao hicho Mkoa umeadhimia pia kuongeza kiasi cha fedha kinachotengwa na halmashauri za wilaya kwa ajili ya ktumika katika afua mbalimbali za lishe kwa watoto chini ya miaka mitano.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa