Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia utekelezaji wa afua za lishe katika halmashauri zao ili kuimarisha hali ya lishe katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo leo tarehe 27 Julai 2021 katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninataka utekelezaji wa afua za lishe upande angalau tuwe kwenye tatu bora kitaifa na sio tunakuwa namba 17 kama hali ilivyo kwa hivi sasa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewasistiza wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuboresha mlo wao kulingana na mahitaji ya kiafya.
Ameeleza kuwa kwa taarifa alizonazo kwa takwimu za mwaka 2018 Mkoa wa Mara ulikuwa na udumavu kwa asilimia 29.2 kwa watoto.
“Udumavu kwa watoto wadogo ni janga la hatari sana ambalo huwezi kuliona kwa haraka ni sawa na bomu linalosubiri kulipuka kwa sababu unasababisha kuwa na watoto ambao hawawezi kufikiri vizuri, kusoma na kujifunza mambo kulingana na umri wao” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amesema kuwa matibabu ya udumavu ni gharama kubwa sana kwa serikali na kuna maradhi mengi yanaayoambatana na lishe duni kwa watu wenye lika mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa kunapokuwa na udumavu kwenye jamii tunategeneza jamii ambayo haiwezi kuwa na tija katika uzalishaji, elimu, na nyanja nyinginezo.
Amemtaka Katibu Tawala kuwaandikia barua wakurugenzi ambao halmashauri zao hazijafanya vizuri katika utekelezaji wa afua za lishe ili watoe maelezo ya kwa nini imetokea hivyo na ahadi yao ya kurekebisha hali hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela ameeleza kuwa Mkoa bado upo nyuma sana katika utekelezaji wa afua za afya na hivyo kunahaja ya watu wote kushirikiana ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe inaonyesha kuwa Mkoa wa Mara upo katika nafasi ya 17 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara jambo ambalo haliridhishi kabisa” alisema Bwana Msovela.
Ameeleza kuwa hiyo inamaanisha watoto wengi wa Mkoa wa Mara wanao udumavu na hatua za haraka zisipochukuliwa hali hii itaendelea.
“Mkoa unalima vyakula vya kutosha, tuna mifugo mingi na samaki pamoja na dagaa kutoka Ziwa Victoria, wananchi wanachohitaji ni elimu zaidi ili waweze kupanga mlo vizuri kulingana na mahitaji ya kiafya” alisema Msovela.
Bwana Msovela ameeleza kuwa changamoto kubwa aliyoiona katika masuala ya lishe ni utoaji wa taarifa, usimamizi na ufuatiliaji wa masuala ya lishe umekuwa mdogo.
Mwaka 2017 serikali iliingia mikataba na Wakuu wa Mikoa yote ili kuhakikisha suala la lishe linasimamiwa vizuri katika mamlaka za halmashauri za wilaya.
Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa halmashauri, Waganga wakuu wa Wilaya, Maafisa Lishe na wataalamu wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa