Mkoa wa Mara umeazimia kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa ya kumaliza Elimu ya Msingi na mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2021.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela wakati akizungumza katika kikao cha wasimamizi wa elimu Mkoa wa Mara cha kutangaza matokeo ya mtihani wa utimilifu (Mock) kwa Kidato cha Nne kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
“Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi ameagiza kuwa wataalamu wa elimu na wote wanaohusika na mitihani wafanye maandalizi yote kwa ajili ya mtihani hiyo na kuhakikisha kuwa Mkoa unashika nafasi nzuri kitaifa” alisema Bwana Msovela.
Bwana Msovela ameeleza kuwa Mheshimiwa Hapi ametaka Mkoa kushika angalau nafasi ya kumi katika mtihani wa kidato cha nne na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Aidha amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kuangalia uwezekano wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi hasa walio katika madarasa ya mitihani ili kuwapunguzia muda wa kutafuta chakula na badala yake watumie muda huo katika maandalizi ya mtihani.
Bwana Msovela ameahidi kuzitembelea shule zote zilizofanya vibaya katika mtihani huo ili kuangalia kinachowakwamisha wanafunzi wao kufanya vizuri katika mtihani.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara Bwana Benjamin Odunga ameeleza kuwa mtihani wa utimilifu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa Mkoa wa Mara ulifanyika kuanzia tarehe 02 Juni 2021 hadi tarehe 18 Juni 2021 ukiwa na lengo la kupima matayarisho ya wanafunzi kwa ajili ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2021.
Akisoma matokeo ya ufaulu wa mtihani huo, Bwana Odunga ameeleza kuwa wanafunzi wamefaulu kwa wastani wa asilimia 78.26 na kuongeza kuwa kwa mwaka huu ufaulu umepanda kwa asilimia 9.47 ukilinganisha na mtihani kama huo wa mwaka 2020 ambapo mkoa ulikuwa na ufaulu wa asilimia 68.79.
Bwana Odunga amewataja wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mtihani huo kuwa ni Irene Thomas Wegesa (Twibhoki), Dorcas Julius Simon (Kowak Girls), Kelly Daniel Chacha (Twibhoki), Emannuel Mrema Emmanuel (Musoma Technical), Jackline Werema Audax (Twibhoki), Paulo Joseph Gidamariri (Musoma Technical), Julius Abel Maginga (Angel House) na Irene Charles Balele (Kowak Girls).
Aidha amezitaja shule zilizofanya vizuri zaidi katika mitihani hiyo kuwa ni Twibhoki (Serengeti), Kitenga Girls (Tarime), Kowak Girls (Rorya), Chief Wanzagi (Butiama), Angel House (Tarime),Girango (Rorya), Dr. John Chacha (Tarime), Makoko Seminary na Amani (Musoma) na Mahende ya mji wa Bunda.
Bwana Odunga amezitaja halmashauri zilizofanya vizuri katika mtihani huo kuwa ni Halmashauri ya Mji wa Bunda ikifuatiwa na Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Halmashauri nyingine kulingana na matokeo hayo ni Halmashauri ya Mji wa Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambayo ilikuwa ya mwisho kwa ufaulu.
Mwalimu Oganga ameeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 23.85 tu ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo na wanafunzi wengine wote waliobakia wamefeli.
“Wanafunzi waliopata daraja sifuri ni 4,874 wakati wanafunzi waliopata daraja la nne ni 12,203. Jumla ya wanafunzi waliopata daraja la nne na sifuri ni wanafunzi 16,077 ambapo ni sawa na asilimia 76.15 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani” ameeleza Bwana Oganga.
Bwana Oganga ameeleza kuwa Mkoa umejiwekea lengo la ufaulu wa asilimia 95 kwa mwaka 2021 katika mtihani huo na kufaulisha kwa asilimia 100 katika mtihani wa taifa ambapo kwa daraja la kwanza hadi la tatu kuwa na ufaulu wa asilimia 50 wakati daraja la nne kufikia asilimia 50.
Bwana Oganga ameeleza kuwa jumla ya masomo 24 yalitahiniwa katika mtihani huo na asilimia 5.34 tu ya watahiniwa wote wamefaulu katika somo la Hisabati huku Kiswahili kikiongoza kwa kufaulisha asilimia 80.91 ya watahiniwa wote.
Bwana Oganga ameeleza kuwa matokeo hayo hayaridhishi ukilinganisha na malengo ya Mkoa na hata ya kitaifa hivyo mkoa unahitaji kuongeza nguvu ya pamoja katika ufuatiliaji wa ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo walimu.
Katika kikao hicho maazimio mbalimbali yalifikiwa ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kutembelea shule zilizofanya vibaya, kutoa chakula shuleni kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani, kuwatumia walimu wenye umahiri katika baadhi ya masomo ili kuwasaidia wanafunzi na kuendelea kufuatilia ufundishaji wa walimu pamoja na mambo mengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa