Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameanza kuchukua hatua mbalimbali katika utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa katika ziara yake mkoani Mara tarehe 4-7 Februari, 2022.
Akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya miradi kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji Mheshimiwa Hapi ameagiza mamlaka zinazohusika kuwasimamisha kazi watumishi saba kutokana na makosa mbalimbali katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mara.
“Hawa wamekuwa wanatuhumiwa kuwa na matatizo mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara, sasa wasimamishwe ili kupisha uchunguzi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Watendaji aliyoelekezwa wasimamishwe ni Bi. Mariam Chacha, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime; Mhandisi Maige James Gibai, Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma; Bi. Maria Nyandoro Chokongoye Mhasibu wa Mapato wa Hamashauri ya Wilaya ya Musoma na Bwana Joseph Orest Luhwa maarufu kama Msuya Afisa katika Idara ya Uvuvi katika Manispaa ya Musoma.
Watendaji wengine ni Bwana Leonard Lukawe Mkau Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Bwana Buzana M. Kazare, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Bwana Nzaya Muhoja, Afisa Manunuzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWASA)
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufuatilia utendaji wa Waganga Wakuu wa Halmashauri za Wilaya za Tarime, Bunda na Musoma, Mweka Hazina wa Manispaa ya Musoma na Afisa Elimu wa Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Aidha katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Musoma, Bunda na Tarime kujieleza kwa maandishi kwa nini Halmashauri zao hazikuomba fedha za miradi ya maendeleo iliyotengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa mujibu wa utaratibu wa fedha za miradi ya maendeleo.
“Tangu tumeanza kutekeleza bajeti ya mwaka huu, huu ni mwezi wa nane sasa tumeanza lakini hawa hawajaomba fedha hizo na miradi hii haijaanza kutekelezwa, wakati wengine wameshaomba na tayari fedha hizo wameshapata na zimeanza kutekeleza miradi iliyopangwa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi ya elimu, afya, nyumba za watumishi na ofisi za Halmashauri.
Fedha ambazo hazijaombwa mpaka sasa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni Tshs. 2,875,000,000/=, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Tshs.2,362,500,000/=, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Tshs. 1,862,5000,000/=.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kufanya uchunguzi katika mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri inayotolewa kwa vikundi vya Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Vijana ili kubaini uwepo wa mikopo hewa na kuwasilisha taarifa kwa Mkoa wa Mkoa ndani ya wiki mbili.
Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri na Wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Wilaya kufanya uchambuzi wa maafisa wanaokaimu ambao baadhi yao wanatuhumiwa kuhujumu uchunguzi unaoendelea kufanyika.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wiki mbili kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha fedha zote za mapato ya ndani ambazo hazijaingizwa benki ziwe zimeingizwa na Wakurugenzi wa Halmashauri wawasilishe wawasilishe majina ya wahusika wote waliokula fedha mbichi na hatua zilizochukuliwa.
“Kwa sasa hivi halmashauri zote zinafedha ambazo zimekusanywa kama mapato ya ndani na hazijaingizwa benki kiasi cha bilioni 1.795 sasa ninataka kupata taarifa ya pesa hizi mbichi zipo kwenye akounti za halmashauri au ni nani aliyekula tushughulike nae” alisema Mheshimiwa Hapi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Meya wa Manispaa ya Musoma, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wakuui wa Taasisi, Wakuu wa Polisi wa Wilaya zote za Kipolisi katika Mkoa wa Mara, Makamanda wa TAKUKURU wa Wilaya na Maktibu Tarafa wote wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa