Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa kununua boti ya doria kwa ajili ya udhibiti wa uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Malima ametoa pongezi hizo tarehe 4 Juni 2020 wakati akizindua rasmi boti ya kisasa iliyonunuliwa na Manispaa ya Musoma kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu.
“Mimi ninawapongeza sana Manispaa ya Musoma kwa kuwa Halmashauri ya kwanza katika Mkoa wa Mara kwa kununua boti itakayoongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria” alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Mkoa wa Mara katika kulinda raslimali za ziwa ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu na ununuzi wa boti hiyo ya kisasa utaimarisha zaidi jitihada hizo na matokeo ni kuongezeka kwa samami na mapato yatokanayo na uvuvi.
Mheshimiwa Malima ameitaka Halmashauri hiyo kuitunza boti hiyo ili itumike muda mrefu kwa manufaa ya wananchi wa Manispaa ya Musoma.
Aidha amempongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Musoma kwa kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kudhibiti uvuvi haramu katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney ameeleza kuwa halmashauri zote mbili za wilaya hiyo zimeongeza sana makusanyo yanayotokana na uvuvi tangia serikali ya awamu ya tano iingie madarakani na hivyo ununuzi wa boti hii unalenga kuimarisha jitihada hizo.
Ameeleza kuwa halmashauri za Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma zinapata jumla ya makusanyo ya shilingi 1.2 bilioni kwa mwaka.
“Kabla ya kuimarisha udhibiti, halmashauri zote mbili zilikuwa zinapata kiasi cha shilingi 160,000 tu kwa mwaka na sasa makusanyo yamepanda maradufu” alisema Dkt. Naano.
Boti hiyo ya kisasa inauwezo wa kuchukua abiria nane na inauwezo wa kukimbia zaidi ya boti za awali zilizokuwa zinatumika katika kudhibiti uvuvi haramu na imenunuliwa kwa gharama ya shilingi milioni 39 ikiwa na vifaa vya usalama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa