Mkoa wa Mara leo tarehe 1 Oktoba, 2022 umeadhimisha Siku ya Wazee Duniani iliyofanyika katika eneo la Nyamwaga, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kuhusisha wawakilishi kutoka Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara katika Siku ya Wazee Duniani ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuunda Baraza la Wazee na Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuzindua mabaraza ya wazee.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mheshimiwa Michael Mtenjele amesema “Ninatoa muda hadi tarehe 30 Desemba, 2022 mabaraza hayo yawe yanafanyakazi na taarifa ya maandishi iwasilishwe katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara”.
Aidha, Mheshimiwa Ntenjele amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii kusimamia uundwaji wa mabaraza ya wazee na kutofautisha kati ya mabaraza hayo na shughuli za utamaduni na mila ili mabaraza haya yafanye shughuli zake kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali.
Mheshimiwa Mtenjele amewaahidi wazee kuwa Mkoa utaendelea kutoa vitambulisho vya matibabu kwa ajili ya wazee na kuagiza Idara za Afya katika Halmashauri za Mkoa wa Mara kuhakikisha zinaimarisha upatikanaji wa dawa katika magonjwa yanayowasumbua wazee.
“Natoa wito kwa Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha dawa muhimu katika magonjwa yanayowasumbua wazee zipo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ili wazee wapate matibabu ya uhakika katika vituo hivyo” alisema Mheshimiwa Mtenjele.
Mheshimiwa Mtenjele pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuwatembelea wazee wanaoishi katika Makazi Maalum ya Wazee eneo la Nyabange na kuwangalia uwezekano wa kuwaingiza katika Mfuko wa TASAF ili waweze kupata pesa ya kujikimu.
Katika risala yao, Baraza la Ushauri la Wazee wa Mkoa wa Mara wamemuaomba Mkuu wa Mkoa wa Mara kuikumbusha Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kuunda Baraza la Wazee kwa mujibu wa sheria na Manispaa ya Musoma, Halmashauri za Wilaya ya Rorya na Bunda kuzindua mabaraza ya wazee.
Baraza la Ushauri wa Wazee pia limeiomba Serikali kuwapatia Pensheni Jamii wazee wote wenye umri mkubwa ili waweze kujikimu katika mahitaji yao ya kila siku.
Aidha, wazee wameitaka serikali kuendelea kutoa elimu na adhabu kwa wanaojihusisha na ukeketaji na kusema ukeketaji ni kosa la jinai na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Risala hiyo pia imeeleza japokuwa wazee wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo lakini kuna tatizo la upatikanaji wa dawa hususan katika magnjwa mengi yanayowakabili wazee jambo ambalo wamesema vitambulisho hivyo kwa sasa haviwasaidii wazee kama ilivyotarajiwa.
Aidha, wazee wameiomba serikali iweke bajeti maalum ya shughuli za mabaraza ya wazee katika Halmashauri zote ili kuwezesha mabaraza ya wazee katika Halmashauri, Kata, mitaa/vijiji yaweze kufanyika kwa mujibu wa miongozo ya serikali.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani mwaka huu ni “Ustahimilivu na mchango wa Wazee ni muhimu kwa Maendeleo ya Taifa”.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Waganga Wakuu wa Halmashauri , Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mara, maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa