Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Moses Kaegele leo ameongoza zoezi la kupanda miti katika Shule ya Sekondari ya Butiama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na kuwataka wananchi kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti.
Mhe. Kaegele ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama ametoa rai hiyo wakati wa zoezi la upandaji miti 1000 katika eneo hilo na kuwataka wanafunzi kuwaelimisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla umuhimu wa kupanda miti kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.
“Watu wakipanda miti kwa wingi, watatunza mazingira na kupata faida mbalimbali za kijamii na za kiuchumi ambazo hazitapatikana kama nchi yetu haitakuwa na miti ya kutosha ili kuhifadhi mazingira yetu” amesema Mhe. Kaegele.
Mhe. Kaegele amewataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri katika kupanda miti na kutunza miti iliyopandwa na kuwa mfano bora katika utunzaji wa mazingira.
Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kuwaonya watu wote wanaojihusisha na biashara ya mkaa na kuni bila ya kuwa na vibali na leseni zinazohitajika kuendesha biashara hiyo na kuahidi kuwa serikali itawachukulia hatua kali watakaobainika kukiuka sheria, kanuni na taratibu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maliasili na Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bwana Emanuel Makoye ameeleza kuwa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ni muhimu sana na kama hakuna uhifadhi wa mazingira hakuna maisha.
“Tunapoyatunza mazingira tunajiepusha na athari nyingi kutokea na tunatunza vyanzo vya maji na tunajilinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi” amesema Bwana Makoye.
Bwana Makoye ameeleza kuwa kwa kupanda miti jamii inapata manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii na kuwataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri katika utunzaji wa mazingira.
Bwana Makoye ameeleza kuwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, jumla ya miti 1000 inategemewa kupandwa katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na misindano, mikongo, mikaratusi na misandawe.
Kwa Mkoa wa Mara maadhimisho haya yamefanyika katika Halmashauri zote tisa kwa kufanya shughuli za usafi wa mazingira, kupanda miti, michezo na kuwasaidia wahanga wa mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Maadhimisho ya miaka 60 kitaifa yanategemea kufanyika tarehe 26 Aprili, 2024 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam yakiwa na kauli mbiu inayosema: Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa letu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa