Mkoa wa Mara leo tarehe 5 Novemba 2021 umetambuliwa kwa mchango wake katika kuhamasisha na kuchanja wananchi chanjo ya UVIKO 19 na kumaliza chanjo kwa wakati na kufanikiwa kuwa Mshindi wa Kwanza katika Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imeutambua mchango huo na kutoa cheti cha utambuzi kwa kufanya vizuri katika awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo ya UVIKO iliyofanyika kuanzia tarehe 5 Agosti, 2021 hadi tarehe 2 Novemba 2021.
Utambuzi huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Prof. Abel N. Makubi katika ufunguzi wa kikao kazi cha Wakurugenzi wa Taasisi, Hospitali za Taifa, Maalum, Kanda, Rufaa za Mikoa Pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa kilichofanyika Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa mawasilisho ya kikao hicho, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Juma Mfanga ameeleza kuwa mbinu mbalimbali zilitumika katika kufikia mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na uchanjaji vituoni, huduma ya mkoba, huduma ya nyumba kwa nyumba, usimamizi shirikishi na ushirikishwaji wa viongozi.
“Katika kuhakikisha kila mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anafikiwa na huduma hii ya chanjo, watoa huduma waliamua kutembelea nyumba moja baada ya nyingine kwenye maeneo mbalimbali ili kutoa elimu na chanjo kwa waliokuwa tayari kuchanjwa” alisema Dkt. Mfanga.
Dkt. Mfanga ameeleza kuwa awali, Mkoa wa Mara ulipokea chanjo za UVIKO 19 dozi 25,000 aina ya Janssen na uzinduzi wa chanjo hii kimkoa ulifanyika tarehe 5 Agosti 2021 na hadi kufika tarehe 4 Oktoba, 2021 chanjo zote zilitumika.
Ameeleza kuwa baadaye Mkoa wa Mara ulipokea chanjo nyingine dozi 9,850 kutoka Mkoa wa Mwanza ambazo zilisambazwa na kutumika kwa wananchi hadi tarehe 12 Oktoba 2021 zilimalizika.
Dkt. Mfanga ameeleza kuwa Mkoa wa Mara pia umepokea dozi 45,969 aina ya Sinopharm ambazo tayari zimeshasambazwa katika vituo vya kutolea huduma na kuanza kutolewa kwa wananchi.
“Hadi sasa wananchi waliochanjwa chanjo ya UVIKO 19 katika Mkoa wa Mara ni 32,479 ambayo ni sawa na asilimia 40 ya dozi 80,819 za chanjo ya UVIKO 19 zilizopokelewa katika Mkoa wa Mara” alisema Dkt. Mfanga.
Awali, vituo 22 vilichaguliwa kutoa huduma ya chanjo ya UVIKO 19 katika Mkoa wa Mara, hata hivyo Mkoa uliongeza na kufika vituo 285 vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Mikoa ya Kanda ya Ziwa inajumuisha mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Tabora na Kagera.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa