Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Musabila Kusaya Juni 30, 2025 amezindua Mpango Mkakati wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika Ukumbi wa Manispaa ya Musoma na kuziagiza Halmashauri kuanzisha mikakati ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kupunguza matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNFPA na Shirika lisilo la kiserikali la WILDAF, Ndugu Kusaya amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Mkoa wa Mara unaweka mkazo katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake.
“Sisi kama Mkoa lazima tuwe vinara katika kupambana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na tutapambana kwa kuwawezesha wanawake kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri pamoja na fursa nyingine za kukuza uchumi wao” amesema Ndugu Kusaya.
Ndugu Kusaya amesema kuwa vikundi vya wanawake katika Mkoa wa Mara vimekuwa vinarejesha kwa wakati mikopo inayotolewa na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha ili kuziwezesha familia kiuchumi.
Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kutenga bajeti ya kujenga nyumba salama ili kuwahifadhi watoto wanaopata changamoto za unyanyasaji na hususan kuhusiana na ukeketaji katika maeneo yao kuweza kuhifadhiwa humo.
Aidha, Ndugu Kusaya ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma shule za msingi na sekondari za kutwa kuchangia chakula shuleni na kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana shuleni.
“Kwa sasa upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wanaosoma shule za kutwa ni kwa asilimia 54 tu, tunawatesa watoto wetu kwa kushinda na njaa wakiwa shuleni” amesema Ndugu Kusaya.
Awali akizungumza wakati akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara Bibi Neema Ibamba amesema mkakati huo utakuwa nyenzo ya kufanyia kazi kwa wadau na Serikali katika kupunguza ukatili kwa wanawake na watoto.
Bibi Ibamba amewapongeza washiriki wote walioshiriki katika uzinduzi wa mpango mkakati huo kwa kushiriki shughuli hiyo na kuwataka kusaidia kutoa elimu katika maeneo yao kuhusiana na mkakati huo.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bi. Jesca Msamba amesema amefurahi kuona jitihada za Serikali katika kuendeleza mapambano ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini nzima.
Bi Jesca amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imejipanga kuhakikisha shabaha ya Serikali katika kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto inafanikiwa na kuwahikisha kuwa Bunda inakuwa na jamii salama isiyo na ukatili.
Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyarigamba A, Mwalimu Deogratius Mungure ambaye pia ni mkalimali wa lugha ya alama amesema jamii inahitaji elimu ya kutosha juu ya ukatili wa kijinsia hasa watoto wenye ulemavu kwa kuwa yapo matukio ya ukatili wanayofanyiwa watoto wenye ulemavu ambayo hayaripotiwi.
Uzinduzi wa Mkakati huo umehudhuriwa na Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Halmashauri, viongozi wa taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya siasa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa