RC AFUNGUA KIKAO KAZI CHA URAGHABISHI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefungua kikao kazi cha uraghabishi kuhusu zoezi la utoaji wa kinga tiba za magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto wenye umri wa miaka 5-14 katika Mkoa wa Mara kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtanda amesema zoezi la utoaji wa kinga tiba kwa watoto litafanyika tarehe 23-24 Novemba, 2023 katika Mkoa wa Mara na kuwahakikishia wananchi kuwa kinga tiba hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu.
“Mimi nitazindua rasmi zoezi la utoaji wa kinga tiba kwa watoto tarehe 23 Novemba, 2023 katika Shule moja ya Manispaa ya Musoma, niwaombe wazazi kuwaruhusu watoto kupata dawa na kuhakikisha watoto wanakula kabla ya kupewa dawa hizi” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Mara na hususan wanaoishi kando kando ya Ziwa Victoria kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kutumia vyoo na maji safi na salama katika matumizi yao ya kila siku.
“Hizi Wilaya ambazo zimetajwa kuwa na magonjwa mengi yanayotokana na kichocho na minyoo tumbo pia zinaongoza kwa kutokuwa na vyoo bora jambo ambalo linaendeleza kuchafua mazingira yao na kuwafanya watoto wa maeneo hayo kuwa hatarini kupata magonjwa” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa kwa siku mbili hizo ambapo dawa kinga zitatolewa, watoto wapewe chakula kabla ya kupewa dawa ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza baada ya kumeza dawa hizo.
Mhe. Mtanda amewataka wataalamu wa Afya na Elimu kusimamia vizuri zoezi hilo ili Mkoa wa Mara uweze kuwafikia walengwa kwa asilimia zaidi ya 100.
Akitoa taarifa za zoezi hilo, Bibi Esther Muya Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika Mkoa wa Mara ameeleza kuwa zoezi hilo linatarajiwa kufanyika tarehe 23-24 katika shule zote za Mkoa wa Mara na kuwahusisha watoto wenye umri wa miaka 5-14.
Bibi Muya ameeleza kuwa japokuwa magonjwa haya hayapewi kipaumbele, lakini yanaathari kubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na kusababisha ulemavu wa muda mrefu, kuathirika makuzi na maendeleo ya mtoto, kuharibika kwa mimba, kupunguza uwezo wa kufanya kazi , hivyo kuleta umasikini kwa mtu binafsi, jamii, na nchi nzima.
Bibi Muya amezitaka athari nyingine kuwa ni pamoja na utapiamlo kwa watoto, upungufu wa damu mwilini, udhaifu unaoweza kukaribisha maradhi mengineyo, presha ya ini, kansa ya kibofu cha mkojo, kuacha shule na upofu.
Ameeleza kuwa kwa ujumla magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ni 17 lakini kwa Mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla magonjw aya minyoo ya tumbo na kichocho yalikuwa hayapewi kipaumbele, yameongeza ulemavu kwa watu na kushindwa kufaya shughuli zao.
Bibi Muya ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa magonjwa haya yanatokana na wananchi kujisaidia katika au jirani na vyanzo vya maji na ndio maana takwimu zinaonyesha Wilaya zilizoathirika zaidi katika Mkoa wa Mara ni Rorya, Musoma na Bunda ambazo zipo kando ya Ziwa Victoria.
Kikao kazi hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominucus Lusasi Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Mwakilishi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa