Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bi. karolina Mthapula amewataka wajumbe wa kamati ya lishe pamoja na Elimu Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa elimu kuhusu urutubishaji wa chakula inasambazwa kwa watoto mashuleni, waalimu, wazazi na wananchi wote kuanzia ngazi ya chini ili kuwepo na uelewa wa umuhimu wa kutumia chakula kilichorutubishwa kwani ni muhimu kwa afya ya watoto.
Bi. Mthapula ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ya Mkoa pamoja kilichowashirikisha Maafisa Elimu kuhusu urutubishaji wa unga wa mahindi unaozalishwa na viwanda vidogovidogo na kati vilivyopo Mkoani Mara, kikao kilichofanyika leo tarehe 31 Mei2021 katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ninaomba wajumbe na wataalamu mliopo hapa tuhakikishe kuwa elimu tunayoipata hapa tunaipeleka kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwani suala la lishe ni suala muhimu kwa afya ya watoto wetu na linapelekea afya ya watoto kuimarika pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu mashuleni”.
Aidha amewataka maafisa elimu kuongeza ufanisi katika kutoa elimu ya lishe mashuleni ili watoto wawe na uelewa stahiki ili nao waweze kwenda kupandikiza elimu hiyo majumbani na kwa jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Frolian Tinuga amesema kuwa Mkoa unaendelea kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kukutana na wadau pamoja na wazalishaji kujadili namna bora ya utekelezaji wa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa chakula lishe kwa wanafunzi elimu msingi unatumika katika shule zote nchini.
“Kama Mkoa tumedhamiria kusimamia na kuhakikisha Muongozo wa lishe mashuleni unatekelezeka kwa kuhakikisha tunaendelea kuhamasisha, kutoa elimu na kuwajengea uwezo wazalishaji waweze kurutubisha vyakula wanavyozalisha sambamba na kuhakikisha wanafunzi wote mashuleni wanakula chakula kilichorutubishwa” alisema Dkt. Tinuga.
Kwa upande wake, mwakilishi wa ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bwana Steven Mtambi amesisitiza ulimaji na ulaji wa mahindi ya njano, maharage, viazi, mbogamboga na matunda kwa shule zenye mazingira yanayowezekana kwani vyakula hivi vina virutubisho ya kutosha na vinasaidia kwa kiwango kikubwa kujenga afya ya watoto.
Bwana Mtambi ameeleza kuwa upungufu wa virutubisho unaweza kusababisha udumavu katika ukuaji wa watoto pamoja na matatizo ya watoto kuzaliwa na mgongo wazi na kichwa kikubwa.
“Asilimia 49% ya watu wa Mkoa wa Mara wana upungufu wa wekundu wa damu unaosababishwa na kukosa lishe bora hivyo nguvu ikiwekezwa katika kuwepo na huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi kutasaidia kuwajengea afya nzuri, kuongeza mahudhuri,kupunguza utoro,kuongeza kiwango cha ufaulu” alisema Bwana Mtambi.
Aidha akimkaribisha Katibu Tawala, Afisa Lishe Mkoa wa Mara Bwana Paul Makali amesema kuwa Mkoa umejipanga kuwajengea uwezo kamati za lishe za Halmashauri ili kuona namna bora ya kuondoa changamoto za lishe katika Mkoa wa Mara.
Bwana Makali amevitaja vyakula vinavyotakiwa kurutubishwa kuwa ni chumvi, mafuta ya kula, unga wa mahindi pamoja na unga wa ngano.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa