Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amefanya ziara ya kutembelea Mgodi wa Barrick North Mara uliopo katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoukabili mgodi huo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa shughuli za mgodi huo kutoka kwa viongozi wa mgodi wa Barrick North Mara wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bwana Apolinary Lyambiko, Mheshimiwa Mzee amesema baada ya kupokea taarifa na changamoto hizo wanajipanga kwa ajili ya kuzitatua.
“Mgodi unataka kupanua shughuli zake na upo tayari kulipa fidia, lakini kuna upinzani mkubwa wa kupata hayo maeneo, inafanyika tathmini lakini inaingiliwa na ujanja ujanja mwingi ambao unasababisha zoezi la kuendelea na uchimbaji likwame” ameeleza Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipotembelea Mkoa wa Mara Mwezi Februari, 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusiana na maeneo yanayohitaji kulipwa fidia ili uchimbaji uendelee.
“Tunaenda kujipanga tuone tunasaidia vipi kuweza kutatua changamoto hii kwa manufaa ya mgodi, wananchi wanaouzunguka mgodi na serikali ambayo ni mbia katika uwekezaji wa mgodi huu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewashukuru viongozi wa mgodi huo kwa taarifa walizotoa ambazo zitasaidia katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoukabili mgodi huo.
Awali wakitoa taarifa zao, viongozi wa Mgodi wa Barrick wameeleza kuwa changamoto nyingine ni wananchi ambao maeneo yao yamefanyiwa tathmini kukataa kuchukua fidia kwa madai kuwa fidia ni ndogo au wanataka wafanyiwe uthamini wa maeneo yao upya baada ya kufanya uwezekezaji zaidi baada ya tathmini ya awali.
Wamezitaja changamoto nyingine kuwa ni uvamizi wa mara kwa mara wa mgodi huo ambao wamedai kwa sasa tangia mwezi Aprili umepungua, lakini awali kulikuwa na wastani wa matukio ya uvamizi matano hadi saba kwa mwezi mmoja.
Wameeleza kuwa wavamizi huingia mgodini makundi makubwa ya watu 50- 70 hususan wakati wa mvua na huingia kulingana na koo zao na inapotokea mtu wa ukoo fulani ameiba madini wanaanza kunyang’anyana wao kwa wao na kujeruhiana lakini wakitoka wanaeleza kuwa wamejeruhiwa na askari wa mgodi.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo viongozi hao wameeleza kuwa uzalishaji katika mgodi huo unaendelea vizuri na kwa mwaka huu kuna dalili kuwa mgodi ukavuka lengo lake katika uzalishaji.
Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Madini Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara na Mthamini wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime.
Huu ni mwendelezo wa ziara za Mkuu wa Mkoa kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais Julai 31 Mwaka huu na kuwasili Mkoa wa Mara Agosti 6, 2022 kuanza kazi.
Kesho tarehe 3 Septemba, 2022 Mkuu wa Mkoa ataendelea na ziara yake ya kujitambulisha katika Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa